Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bw. Simon Berege (kushoto) akimwonesha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo mapema leo tarehe 30 Agosti, 2019 katika kata ya Ntobo.
Kaimu Mkurugenzi wa SUMA JKT Kaptain Fabian Buberwa (kulia) akimuelezea Waziri wa Ujenzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi namna wanavyotekeleza mradi wa kujenga makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack wakiangalia ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala leo tarehe 30 Agosti, 2019.
Sehemu ya ujenzi wa majengo ya Makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala inavyoonekana.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telacl na viongozi wengine wakiendelea kukagua ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza na viongozi na watendaji katika eneo la ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
****************
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amesema anaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na miradi inayotekelezwa na SUMA JKT kanda ya Ziwa.
Dkt. Mwinyi akiwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na SUMA JKT pamoja na makampuni mengine yaliyo chini ya Wizara hiyo kanda ya Ziwa mapema leo tarehe 30/08/2019 katika Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga amesema kwa kiwango kikubwa ameridhishwa na kazi zinazofanywa na sehemu kubwa kazi zimekwenda kwa kiwango kinachotarajiwa na kuwa changamoto zilizopo zitafanyiwa kazi.
“Niwahakikishie Mikoa na Halmashauri zinazohusika na miradi inayotekelezwa na SUMA JKT changamoto zote zitafanyiwa kazi” amesema Dkt. Mwinyi.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais John Magufuli kwa kuiamini kampuni hiyo iliyo chini ya Wizara yake na ndiyo sababu ya yeye kufanya ziara hiyo ili kuhakikisha imani hiyo inadumu pamoja na kuwaomba viongozi wote wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kuiamini.
Aidha, amewataka SUMA JKT kuongeza kazi ya ziada mara watakapopata fedha ili kukamilisha jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambalo ujenzi wake umesimama kutokana na changamoto ya fedha.
Naye Mkurugenzi wa SUMA JKT Kanali Rajab Mabele amesema kuwa, kampuni hiyo imepiga hatua kubwa hasa katika nyanja ya ujenzi lakini pia inajihusisha na kazi nyingine mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji.
Awali, akimkaribisha Dkt. Mwinyi Mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemuomba kupitia kampuni ya SUMA JKT kuangalia jinsi ya kuwa na miradi ya kuvuna maji ili wananchi waweze kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji.
“Pamoja na kiangazi kilichopo, tunapata mvua nyingi sana na tunavuna mpunga unaoweza kulisha nchi yote, sasa tuone namna bora ya kuvuna hayo maji na tayari baadhi ya wananchi wameshaanza kuchimba mashimo makubwa ya kuvuna maji, tumeona kama Mkoa tufanye hilo ili wananchi wetu waweze kupata mpunga” amesema Telack.