JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof Ibrahim Juma ameeleza kuwa aliyekua Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli alimuagiza aliyekua Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kuwapatia Mahakama kiwanja ili waweze kujenga Ofisi za Makao Makuu ya mhimili huo.
Prof Ibrahim ameyasema hayo wilayani Chato Mkoani Geita wakati wa kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha Hayati Dk Magufuli ambacho kilitokea Machi 17 mwaka 2021.
Akizungumza na viongozi na wananchi waliojitokeza katika Misa hiyo, Jaji Mkuu amesema Hayati Dk Magufuli alimuita ofisini kwake kumuuliza Mpango wa Mahakama kuhamia jijini Dodoma na ndipo alipomtaka Mkurugenzi wa Jiji Kunambi kuwezesha upatikanaji wa kiwanja kwa ajili ya kujenga Ofisi hizo.
” Nakumbuka Mahakama ilikua Muhimbili wa mwisho kuhamia Dodoma, Bunge lilishatangulia halafu Serikali ikafuata, Siku moja Hayati Dk Magufuli akaniita ofisini kwake akaniambia Nchi imehamia Dodoma nyie Mahakama mna Mpango gani? Nikamwambia sisi tunategemea kuwezeshwa ndio tuhame.
Ndipo akamuagiza Mkurugenzi wa Jiji ambaye Sasa hivi ni Mbunge, Godwin Kunambi ambaye alitafuta maeneo mawili makubwa kwa ajili ya ujenzi wetu. Tunashukuru tuliwezeshwa na leo jengo limefikia sehemu nzuri Sana,” Amesema Jaji Mkuu Prof Ibrahim.