OR- TAMISEMI
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Grace Tendega amesema Hawajaridhishwa na matumizi ya fedha katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Mhe. Tendega amesema kuwa gharama iliyotumika katika utekelezaji wa ujenzi ni kubwa ukilinganisha na majengo ambayo yamejengwa, pia majengo ambayo yamekamilika hayana viwango huku mengine yakihitaji ukarabati hata kabla hayajaanza kutumika.
Kauli hiyo imetolewa Machi 18, 2022 katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ilipotembea na kukagua ufanisi wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mbarali.
“Ujenzi wa hopitali ya Mbarali hatujaturidhisha kabisa,gharama iliyotumika imetupa wasiwasi mkubwa haiendani na uhalisia, pili majengo hayana ubora unakuta mengine kuta zina nyufa” Amesema Mhe. Tendega.
Ameongeza kuwa dhana ya kutumia force account katika utekelezaji wa miradi ni kupunguza gharama kwa kuzingatia ubora katika utekelezaji lakini, ameshangazwa na gharama kubwa ambayo imetumika katika ujenzi huo ilhali umetekelezwa kupitia force account.
Kutokana na mapungufu yaliyobainishwa ,Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt.Switbert Mukama ameihakikishia Kamati kuwa itatekeleza maagizo yaliyotewa na Kamati kuhusu ujenzi wa hospotali hiyo.
Katika hospitali hiyo majengo yaliyokalimika ni jengo la utawala na wagonjwa wanje, jengo la dawa, jengo la kufulia nguo, jengo la chanjo, jengo la jenereta pamoja na jengo la mionzi, jengo la maabara, wodi ya wazazi , wodi ya watoto, wodi ya wanaume na wanawake yapo katika hatua ya umaliziaji.