Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Kanda ya Kati Sonia Mkumbwa akisisitiza jambo kwenye kikao hicho..
Taswira ya mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mada.
Kikao kazi kikiendelea.
Mada zikiendelea.
Mkaguzi wa dawa Saraphiana Cleophace akitoa mada kuhusu udhibiti wa bidhaa za Tumbaku.
Washiriki na mgeni rasmi wakiwa katika picha ya pamoja.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imepiga marufuku kutumia bidhaa za tumbaku katika maeneo yasiyo rasmi ili kulinda afya za jamii.
Agizo hilo lilitolewa katika kikao kazi cha kutoa uelewa wa Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku kilicho
wakutanisha TMDA, Uongozi wa Wafanyabiashara na
Viongozi wa ngazi ya mkoa na
Manispaa ya Singida.
Akizungumza kwenye kikao hicho Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Kati Sonia Mkumbwa alisema ni jambo zuri kwa watumiaji wa bidhaa za tumbaku kutengewa maeneo maalumu ya matumizi ya bidhaa hizo ili kuondoa matumizi hayo maeneo ya hadharani ili kusaidia kulinda afya za watu wengine ambao hawatumii tumbaku.
“Ni vizuri sasa watumiaji wa bidhaa za tumbaku (wavutaji wa sigara) kutengewa maeneneo maalumu ya kutumia bidhaa hizo ambazo zitawekwa vibao vikavyoyaonesha maeneo hayo ili iwe rahisi kutambulika badala ya hivi sasa ambapo matumizi yake yamekuwa yakifanyika hadharani ” alisema Mkumbwa.
Katibu Tawala Msaidizi upande wa Uchumi na Uzalishaji, Lanslaus Choaji Mkoa wa Singida akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati akifungua kikao kazi hicho alisema mafunzo hayo ni ya muhimu sana.
Choaji alitumia nafasi hiyo hiyo kuwakaribisha na kuwashukuru wadau wote kwa kuweza kuhudhuria kikao hicho muhimu chenye lengo la kupeana uelewa wa shughuli za udhibiti wa matumizi ya bidhaa za tumbaku katika mkoa wa Singida Pamoja na utekelezaji wake unaofanyika nchi nzima.
“Nafahamu kuwa TMDA imekasimishwa jukumu hili la udhibiti wa matumizi ya bidhaa za tumbaku na Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya Afya Aprili 30, 2021. Hivyo basi, nawapongeza sana kwa kulipokea jukumu hili na bila kuchelewa mmeweza kuandaa mpango kazi wa miaka mitatu 2021/2022 hadi 2023/2024) wa utekelezaji wa shughuli za udhibiti wa bidhaa hizi lengo likiwa ni kupunguza ama kuzuia matumizi ya bidhaa za tumbaku na madhara makubwa ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa hizi” alisema Choaji.
Alisema tafiti zinaonesha matumizi ya bidhaa za tumbaku yamekuwa yakiongezeka kwa kasi ulimwenguni ambapo chimbuko lake ikiwa katika nchi zilizoendelea lakini kwa sasa imebanika kuwa matumizi makubwa ya bidhaa hizi yako katika nchi zinazoendelea.
“Takwimu zimebainisha kuwa zaidi ya watu bilioni 1.3 ya watumiaji wa bidhaa za tumbaku duniani wako katika nchini zetu zinazoendelea. Aidha, tafiti hizo zimebainisha madhara makubwa yaliyoelezwa ni pamoja na vifo vya zaidi ya watu milioni 7 duniani kila mwaka vinavyosababishwa na magonjwa yanayotokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.
Wakati huo huo TMDA imetoa mafunzo kwa watumishi wa Sekta ya Afya mkoani hapa yanayohusu utoaji wa taarifa za madhara au matukio yanayohisiwa kusabibishwa na Matumizi ya Dawa,Vifaa Tiba,Vitendanishi na Chanjo.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye alikuwa awe mgeni rasmi, Elikana Lubango alisema mafunzo hayo yatakwenda kutatua Changamoto kubwa ya utoaji wa taarifa juu ya madhara yanayojitokeza kutokana na matumizi ya dawa.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Kanda ya Kati Sonia Mkumbwa amewahimiza Wafamasia kote nchini kuhakikisha wanaingiza au kuuza dawa ambazo zimesajiliwa na TMDA ili kuepusha madhara kwa watumiaji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema yatawasaidia katika majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutoa huduma nzuri na kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya Dawa na Vifaa Tiba.