Na Dotto Mwaibale,
Singida.
KAMATI ya
Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imekagua miradi 11 ya maendeleo
iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya hiyo na
kuridhishwa na matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya
utekelezaji wake.
Akizungumza kwa
nyakati tofauti juzi na jana wakati kamati hiyo ikikagua miradi hiyo ikiwa ni
utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wa chama
hicho wilayani humo Mika Likapakapa
alisema ameridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo katika halmashauri
hiyo licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo.
“Kwa kweli
tunawapongeza kwa kuitendea haki miradi hii ambayo Serikali inatumia fedha
nyingi kuitekeleza hivyo nawaombeni kuendelea kutumia nguvu hiyo hiyo ya ushirikiano ya kufanya kazi hii ya kutekeleza
miradi yetu yote kwenye wilaya yetu,” alisema Likapakapa.
Likapakapa alitumia
nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na
kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza
kutokana na umuhimu wake.
Alisema Serikali
inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi na ni wajibu wa wananchi nao
kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za
maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Likapakapa aliwaomba
wahandisi wa wilaya hiyo kujenga tabiaya kutembelea mara kwa mara na kukagua
miradi inayojengwe ili ikamilike kwa wakati.
Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo Ally Mwanga aliwataka wakandarasi waliopewa kutekeleza miradi
kuikamilisha kwa wakati kabla walivyo saini kwenye mikataba yao na si
vinginevyo.
“Tunawaomba
wakandarasi mliyopewa kazi ya kujenga miradi hii jengeni ndani ya muda
mliokubaliana katika mkataba na kazi hiyo iwe ya viwango kulingana na thamani
ya fedha mliyopewa” alisema Mwanga.
Wajumbe wa kamati
hiyo wakizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo waliwapongeza Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo, Justice Kijazi, Mkuu wa Wilaya Jerry Muro, Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya hiyo Ally Mwanga pamoja na wakuu wa idara na viongozi mbalimbali
kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo
kwa uaminifu
Baadhi ya
miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo ni utekelezaji wa mradi wa maji Ikungi
ambao gharama yake ni Sh.313,718,795.75,
Utekelezaji wa mradi wa Maji Kata ya Ihanja wenye thamani ya Sh.
368,813,749.50, Ujenzi wa Miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Ikungi ambao
ulitengewa kiasi cha Sh.1,500,000,000, Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu Shule ya
Msingi Mandimu iliyopo Tarafa ya Mungaa ambaouligharimu Sh. 20 Milioni.
Miradi mingine
iliyokaguliwa na kamati hiyo ni Utekelezaji wa miradi ya barabara za
Utaho-Makiungu na Siuyu- Nali na Makotea ambao utagharimu jumla
Sh.488,301,400.00, Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA, Kituo cha Afya cha
Kata ya Kinyampembee na Ntuntu pamoja na Mradi wa Umeme wa Kata ya Makiungu
ambao utazinufaisha kaya 50.
Leo Kamati ya
siasa ya Mkoa wa Singida itafanya ziara ya namna hiyo katika Halmashauri za
Wilaya ya Ikungu na kukagua miradi iliyopo
Kata ya Irisya.