Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasili makao makuu ya Halmashauri ya Babati Vijijini kuweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la makao makuu ya halmshauri hiyo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la makao makuu ya halmshauri hiyo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi, watumishi pamoja na wananchi mbalimbali wa halmashauri ya Babati Vijijini mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la makao makuu ya halmshauri hiyo
………………………………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 16 Machi 2022 amefungua Daraja la Magara pamoja na barabara unganishi ya kilometa 5.2 inayoenda sambamba na daraja hilo lililopo Wilaya ya Babati mkoani Manyara. Ujenzi wa Daraja hilo umegharimu shilingi bilioni 11.92.
Akizungumza mara baada ya kuzindua daraja hilo Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Magara na Manyara kwa ujumla kwa mradi huo mkubwa uliofungua fursa za kiuchumi.
Makamu wa Rais amewataka wananchi wa eneo hilo kuacha mara moja shughuli pembezoni mwa mto ikiwemo kuchimba mchanga na shughuli za kilimo ili kuepusha mto kuhama na daraja kuharibika. Amesema kila mmoja anapaswa kulinda mazingira na miundombinu inayotekelezwa na serikali katika maeneo yao.
Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Manyara kuachana na mila potofu zinazopelekea unyanyasaji wa kijinsia na ukatili kwa wanawake na watoto. Amesema mkoa huo unakumbwa na changamoto ya matukio ya ukatili hali inayorudisha nyuma uwezo wa kujiamini husasani kwa wanawake.
Aidha amewaasa wananchi wa Manyara kujiepusha na migogoro ya ardhi na kujichukulia sheria mkononi. Amesema utatuzi wowote wa migogoro ya ardhi unapaswa kufuata taratibu za kisheria. Pia Makamu wa Rais ameiagiza wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na wizara zingine husika kushughulikia mara moja mgogoro uliopo baina ya mwekezaji ambaye ni Manyara Estate na wananchi wa Magara.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameweka jiwe la msingi mradi wa jengo la makao makuu ya halmashauri ya Babati vijijini. Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 3.2 unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka 2022.
Makamu wa Rais amewaasa watendaji wa serikali kutumia vema fedha za serikali zinazopelekwa katika miradi. Aidha amewaasa watumishi kuwa na nidhamu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuwahudumia wananchi kwa upendo.
Aidha Makamu wa Rais amewataka wakandarasi ambao ni Suma JKT kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango na ubora uliopangwa. Makamu wa Rais amewataka SUMA JKT kujirekebisha katika utekelezaji wake ikiwemo kuchukua muda mrefu katika kukamilisha miradi ili kuendelea kuaminiwa na serikali.