**************************
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amewataka waendesha pikipiki maarufu bodaboda kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani kwa lengo la kujiepusha na ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.
IGP Sirro amesema hayo akiwa Buseresere mkoani Geita wakati aliposimamisha msafara wake kwa lengo la kuzungumza na wananchi wa eneo hilo ambapo IGP Sirro amesema kuwa, kutokana na jitihada zinazofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amewapatia wakazi wa eneo hilo gari moja itakayosaidia kutoa huduma za kipolisi kwa haraka.
Aidha, IGP Sirro ameahidi kutoa kiasi cha shilingi laki tano kwa mwananchi yeyote atakayefichua mhalifu anayetumia silaha ya moto.
Naye kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza SACP Ramadhani Ng’anzi amesema kuwa, Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limeendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoa wa Geita kwa kufanya Operesheni za pamoja za kudhibiti uhalifu na wahalifu.