Na.Alex Sonna,Kondoa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.Binilith Mahenge amewatahadharisha wananchi pamoja na mkandarasi anayejenga mradi wa maji katika kitongoji cha Fai kijiji cha Ntomoko wilayani Kondoa kutoharibu mradi huo kwani yeyote atakaethubutu kufanya hivyo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Imeelezwa kuwa mradi huo ambao Chanzo chake ni chemichemi yenye uwezo wa kuzalisha lita laki 5 na elfu 27 kwa siku pindi utakapo kamilika utahudumia wananchi elfu 21 kutoka katika vijiji vinne vya wilaya ya Kondoa na Chemba.
Dkt,Mahenge amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kisha kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Ntomoko ambapo mbali na kuwahakikisha maji kutoka mapema mwezi Octoba mwaka huu pia amesema kuwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli ametenga Jumla ya Shilingi Bilion 2.2 kwa ajili ya kuhakikisha wananchi hao wanapata maji, hivyo mtu yeyote atakaefanya ubadhilifu katika maradi huo atawajibishwa.
“Mimi ndio Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,nimekuja kuwahakikishia kuwa safari hii maji mnapata,sasa hivi tuna watu wa uhakika na nimeongea na mkandarasi amenihakikishia kuwa hadi kufikia mwezi wa kumi maji yatakuwa yanatoka hapa,watakaoharibu tunawasweka wote ndani,hakuna mtu kupona hapa,lazima wahakikishe mradi huu unakamilika”Alisema
Aidha pia Dkt,Mahenge amewaomba wazee na Serikali ya kijiji hicho kuwasimamia wananchi kutofanya shughuli za kibinadamu jirani ya chanzo hicho ili kutosababisha maji kupungua
“Wazee wa eneo hili na Serikali ya Kijiji hapa naombeni muwaambie wananchi wenu waache kuharibu chanzo hiki cha maji,kwani itafikia kipindi maji yatapungua na mwishowe yatakauka kabisa,na kama ikitokea hivyo nyie wote mtakosa maji,kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake hakikisheni hamfanyi shughuli za kibinadamu kwenye eneo hili”Aliongeza
Kwa upande wake Mhandisi John Orest kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) yeye amesema kuwa mkandarasi wa mradi huo amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuanzia June 7 mwaka huu na tayari amekwisha lipwa jumla ya Shilingi Milioni 680 sawa na asilimia 6.4 ya fedha zote
Wananchi wa eneo hilo wamempongeza Rais Dkt.Magufuli huku wakisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawaondolea adha kubwa walioyonayo ya kuasafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo muhimu ya Maji.