Maandalizi ya uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma kilichopo Mkoani Mtwara yameshika kasi ambapo mkandarasi atakayefanya kazi ya uchukuaji wa data hizo (Kampuni ya Africa Geophysical Services – AGS) kwa niaba ya mwendeshaji wa Kitalu cha Ruvuma (Kampuni ya ARA Petroleum) anaendelea na kazi ya kusafisha njia zitakazotumiwa wakati wa uchukuaji data.
Aidha, mkandarasi huyo ameendelea na kazi ya kutoa elimu kuhusiana na kazi tarajiwa kwa wanakijiji wanaoishi eneo la mradi.
AGS ilianza maandalizi ya kazi hii mwishoni mwa mwaka jana na inatarajiwa kuanza uchukuaji wa data hizo za mitetemo za 3D siku za usoni, ikihusisha eneo la kilomita za mraba 334. Magari ya kusafisha njia zitakazotumiwa wakati wa uchukuaji wa data hizo yanaendelea na kazi eneo la mradi.
Hadi sasa, kupitia kazi za maandalizi ya uchukuaji wa data tajwa, watanzania zaidi ya 60 wameweza kuajiriwa katika mradi na makumi ya watoa huduma wakitanzania wamenufaika.
Kazi ya uchukuaji wa data za mitetemo za 3D inayotekelezwa na ARA Petroleum kupitia AGS ni miongoni mwa kazi zinazopaswa kutekelezwa kisheria kwa mujibu wa masharti ya leseni.
Kazi zingine ni kuchimba kisima kimoja cha utafutaji cha Chikumbi 1 na kukamilisha majadiliano ya mauziano ya gesi (gas terms) kulingana na Mkataba wa Uzalishaji wa Ugawanaji Mapato wa Kitalu cha Ruvuma.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambaye ndiye mshika leseni za vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa niaba ya Serikali, anafanya kazi bega kwa bega na mwendeshaji wa Kitalu hicho kuhakikisha masharti ya leseni yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi zinazoendelea katika Kitalu cha Ruvuma na vitalu vingine vilivyo katika hatua ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini hufanywa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) kwa mujibu wa Sehemu ya 12(2) ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.
Miongoni mwa maeneo yanayoangaziwa na PURA wakati wa kaguzi za ufuatiliaji ni masuala ya kitalaamu na ushirikishwaji wa watanzania katika kazi zinazotekelezwa.
Kazi ya kusafisha njia zitakazotumiwa wakati wa uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma ikiendelea kwa kutumia gari maalum ijulikananyo kama mulcher
Baadhi ya magari yatakayotumiwa kuchukua data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma yakiwa tayari kabisa katika kambi ya AGS iliyopo Mtwara
Kazi ya tathmini ya uharibifu wa mazao katika Kijiji cha Maranje Kilichopo Kata ya Mtiniko. Pichani ni wathamini kutoka kampuni ya Tansheq, mwenyekiti wa Kijiji cha Maranje na baadhi ya wanakijiji ambao maeneo yao yamepitiwa na magara yanayosafisha mistari itakayotumiwa wakati wa kazi ya uchukuaji wa data.
Mjiolojia kutoka TPDC, Bw. Lucas Luhanga (mwenye kofia nyeupe) akifanya mahojiano na mthaminishaji, Bw. Eric kutoka kampuni ya Tansheq kuhusiana na rekodi iliyofanyika. Katikati ni Bw. Issa Nangoma, mwenyekiti wa Kijiji cha Maranje iliyopo Kata ya Mtiniko (Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara)
Gari aina ya bulldozer ikisafisha njia zitakazotumika wakati wa uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma