Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Kassim Majaliwa akikaribishwa na Mkurugenzi wa NMB Bank – Albert Jonkergouw kwenye futari maalumu iliyoandaliwa na NMB jijini Dodoma kwaajili ya wateja na wadau mbalimbali.Pembeni ni Spika wa Bunge – Job Ndugai
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Kassim Majaliwa akihutubia wageni mbalimbali waliohudhuria Futari iliyoandaliwa na NMB.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya NMB na wageni mbalimbali waliohudhuria Futari iliyoandaliwa na NMB.
……………………………………………………..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaja benki ya NMB kuwa ni taasisi inayopaswa kuigwa kwa ubora wa huduma akisifia namna walivyoweka mizizi katika maeneo ya vijijini ambako wengi hawajafika.
Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi katika hoteli ya New Dodoma wakati benki ya NMB ilipowakutanisha wadau kutoka mkoani hapa kwenye futari maalum kwaajili ya Mwezi Mtukufu.
Waziri Mkuu alisema benki hiyo inaisaidia serikali katika juhudi za maendeleo hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika uchumi wa kati hivyo anaomba Watanzania kwa Umoja wao kudumisha, amani, upendo na mshikamano ili kufikia malengo.
Alisema serikali ambayo ina hisa ndani ya benki hiyo, itaendelea kushirikiana nao pale wanapoona inafaa kufanya hivyo lakini akawataka waendelee kuboresha zaidi huduma zao katika maeneo ambayo hawajafika.
“Siyo dhambi nikisema mnaongoza kwa kutoa huduma bora, nawashukuru kwa kujikita katika taasisi kama mashule ambako mmesaidia kupeleka madawati na vitabu, lakini nafurahi kusikia mmeanza kufadhili hadi kwenye michezo, nawapeni hongera, tutaendelea kuwatia moyo na popote mlipo,” alisema Majaliwa.
Katika ukaribisho wake, Mkurugenzi wa benki ya NMB Albert Jonkergouw alisema benki hiyo inajishusha kwa kuwakumbuka waumini katika kipindi hiki ambacho wanahitaji kuwa karibu na muumba wao hivyo wanaungana katika tendo hilo jema.
Jonkergouw alisema wataendelea kufanya hivyo na kufuata taratibu za huduma za fedha nyingi ikiwemo kuwasogezea zaidi huduma watu ambao wamekuwa wakizitafuta kwa gharama lakini akasema katika futari watahitimisha Mei 31 mkoani Tabora lakini kila mkoa wanatumia nafasi hiyo kuwaalika na wawakilishi kutoka maeneo ya jirani.