Afisa Msimamizi Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Julieth Shehiza (kushoto) akimuelimisha Mlipakodi mkoani Dodoma kuhusu umuhimu wa kuwa na mashine ya kodi ya kielektroniki ya kutolea risiti (EFD) wakati alipomtembelea katika duka lake wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Dodoma.
Mbunge na Balozi wa Kodi wa hiari, Mhe. Zulfa Omary Mmaka (kushoto) pamoja na Afisa Msimamizi Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. James Ntalika wakiangalia Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) mkoani Dodoma wakati walipomtembelea katika duka lake wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Dodoma.
Mbunge na Balozi wa Kodi wa hiari, Mhe. Zulfa Omary Mmaka (kulia) akimhimiza mlipakodi wa mtaa wa Ilazo mkoani Dodoma kuhusu kutoa risiti za EFD kwa wateja wake anaowauzia bidhaa mbalimbali wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Dodoma.
***********************
Na. Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka Wafanyabiashara mkoani Dodoma ambao mpaka sasa hawana Mashine za Kodi za Kielektroniki za kutolea risiti yaani EFD kuhakikisha kwamba wananunua mashine hizo na kutoa risiti kutokana na mauzo wanayoyafanya kwa wateja wao.
Wito huo umetolewa mjini Dodoma na Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa TRA, Bw. James Ntalika wakati wa mwendelezo wa Kampeni ya Utoaji Elimu kwa Mlipakodi ya kuwatembelea Wafanyabiashara katika maeneo yao ya kazi maarufu kama Mlango Kwa Mlango kwa lengo la kuwapatia elimu ya kodi ikiwemo kusikiliza na kuzitatua kero zao.
Ntalika amesema kwamba, baadhi ya changamoto walizozibaini katika kampeni hiyo ni baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa na mashine za EFD jambo linaloikwamisha TRA kukosa mapato yatokanayo na biashara zao na pia kuna baadhi yao hawana Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kuwataka kufika ofisi ya TRA mkoani hapo ili waweze kusajiliwa na kupatiwa TIN.
“Kuna wafanyabiashara wa hapa mjini Dodoma wanastahili kuwa na mashine za EFD lakini hawana mpaka sasa, hivyo tunawashauri wanunue na kuzitumia mashine hizo na pia wajitahidi kutoa risiti ipasavyo na wanunuzi tunawahimiza kudai risiti wakati wote wanapofanya manunuzi”, alisema Ntalika.
Kwa upande wao baadhi ha Wafanyabiashara wameiomba Serikali iweze kuwapunguzia baadhi ya kodi kutokana na biashara zao kuwa ngumu, huku wengine wakipongeza zoezi la TRA kuanza kuhimiza wananchi juu ya matumizi ya programu ya HAKIKI STEMPU ambapo wananchi wanahimizwa kupakua katika simu zao janja na kuanza kufanya uhakiki wa Stempu za Kodi za Kielektroniki yaani ETS katika bidhaa mbalimbali kama vile maji, pombe, sigara lengo ni kwa ajili ya kulinda afya zao kupitia programu hiyo ya TRA.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea na kampeni yake ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango ikiwa na lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kukuza wigo wa walipakodi nchini ambapo zoezi hilo kwa sasa lipo katika mikoa ya DODOMA na MANYARA kuanzia tarehe 07 Machi, 2022 hadi tarehe 19 Machi, 2022.