OR-TAMISEMI
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia umetekeleza maagizo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe aliyoyatoa Desemba 27, Mwaka 2021 ya kukamilisha ujenzi wa madarasa matatu ya awali ya shule ya sekondari katika Kisiwa cha Jibondo kwa ajili ya wanafunzi 53 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.
Prof. Shemdoe wakati wa ziara yake Wilayani Mafia Tar 09.03.2022 na kufika kisiwani Jibondo amemahkuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia na kutosha Sh. Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa sekondari itakayochukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi sita wa visiwa vya Jibondo, Chole na Juwani.
Akizungumza katika ziara yake, Katibu Mkuu huyo amesema alilazimika kuagiza kujengwa kwa madarasa matatu ya awali kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi hao baada ya kuchaguliwa Shule za Sekondari Kitomondo na Kilindoni ambazo ziliwalazimu kuvuka kwa maji ili kuzifikia shule hizo.
Kabla wanafunzi hao hawajaanza kusomea katika shule ya Jibondo walianza kusoma kwenye shule ha Msingi Jibondo wakisubiria kukamilika kwa madarasa yao ili waweze kuhamia rasmi na kuanza masomo yao ktk shule yao ya Sekondari.
Prof. Shemdoe ameagiza uongozi wa Wilaya ya Mafia kuendelea kusimamia ujenzi wa majengo yaliyobakia ili ifikapo Julai, Mwaka 2022 na ikamilike kwa ubora unaotakiwa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhandisi Martin Ntemo amesema kazi hiyo ilifanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu mpaka kukamilika kwake.
“Tulipoona changamoto ya upelekaji wa vifaa unaathiri zoezi la ujenzi tuliomba Kivuko cha Jeshi ambacho ndicho kilichotusaidia kupeleka vifaa vyote vya ujenzi na hata gari ya kwanza kufika Jibondo imepelekwa na kivuko hicho kwa ajili ya kuchukua vifaa kutoka feri mpaka eneo la ujenzi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wilaya ya Mafia Kassim Ndumbo, amesema walipokea fedha za kujenga madarasa 10, nyumba za walimu ( 2 in 1 ) mbili, maabara tatu, jengo la utawala pamoja na vyoo vya walimu na wanafunzi.
Mkazi wa Jibondo, Aisha Mwindadi, ameshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea shule kwenye kisiwa hicho na imeokoa Sh.2,000 walizokuwa wakitoa kila siku kwa ajili ya watoto wao kupanda boti kwenda na kurudi shule.
Ziara ya Prof. Shemdoe Kisiwani Mafia ni ufuatiliaji wa maagizp aliyoyatoa Dec 27,2021 kisiwani humo ambapo ni miongoni mwa maeneo magumu kufikika na huu umekua umataratibu wake kila mahali anapotoa maagizo kufuatilia utekelezaji wake.