Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam wakati akieleza Mafanikio ya mwaka mmoja ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita. Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam akieleza Mafanikio ya mwaka mmoja ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita.Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam wakati akieleza Mafanikio ya mwaka mmoja ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita.
******************
Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini hali iliyopelekea mapinduzi makubwa katika sekta ya uwekezaji wa viwanda na biashara.
Akiongea leo Machi 10, 2022 Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita kwa kipindi cha mwaka mmoja madarakani, Dk Kijaji amesema ndani ya mwaka mmoja viwanda vipya takribani 327 vimeanzishwa sehemu mbalimbali hapa nchini.
“ Takwimu zinaonyesha katika mwaka mmoja wa uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, viwanda vipya 327 vimeanzishwa ambavyo vinajumuisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, aidha, mara kadhaa nimepokea maelezo kutoka kwa Rais Samia aliyenitaka kuboresha mazingira ya wawekezaji ikiwemo kukomesha urasimu katika kuhudumia wawekezaji, kuimarisha mazingira ya biashara na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima vya kibiashara baina ya Tanzania na nchi jirani ”, alisema Dkt. Kijaji.
Akiongelea idadi ya wawekezaji kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Machi, 2021 mpaka mwezi Februari 2022. Serikali imeweza kuvutia na kusajili jumla ya miradi 294 yenye thamani ya shilingi Trilioni 118.75 miradi ambayo itatoa ajira rasmi zaidi ya 62,000 kwa Watanzania.
“ Idadi hii ya nafasi za ajira ni kubwa kuwahi kuandikishwa na kusajiliwa na kituo chetu cha uwekezaji Tanzania tangu kuanzishwa kwa Taifa letu, hii inatiwa nguvu na kauli ya Rais wetu Samia ambaye aliwahi kusema ‘Watanzania tunawahitaji wawekezaji, zaidi ya wawekezaji wanavyotuhitaji sisi’ ambapo yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wawekezaji kuja”, aliongeza Dk Kijaji.
Dk Kijaji pia aliongelea ushiriki wa Tanzania kwenye maonyesho ya kibiashara ya kimamaifa maarufu kama Dubai Expro 2020 kama moja ya jambo kubwa lililofanikiwa ambapo mataifa 192 yalishiriki maonyesho hayo na Watanzania takribani 200 walihudhuria kati ya wajumbe 500 walioshiriki siku ya maadhimisho wakiongozwa na Rais Samia.
Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kudhibiti bei ya mafuta ya kupikia na sukari ambayo alisema haitabiriki kwa muda mrefu sasa, Waziri Kijaji alisema kwamba serikali imelipa uzito suala hilo, hivyo kuanzisha kongani za viwanda Dakawa, Morogoro ambapo maboresho makubwa yatafanyika kuanzia kwenye mbegu bora ili kuzalisha mafuta ya kutosha na kupata suluhisho la kudumu.
“ Mfumuko wa bei tulionao kwenye eneo la mafuta na sukari unasababishwa na sisi kutokujitosheleza na uzalishaji wetu wa ndani, hivi sasa tunategemea sukari na mafuta kutoka nje lakini tutakapoanza kuzalisha wenyewe hali hiyo itaisha”
Dk Kijaji anatoa wito kwa Wanzania kutoa ushirikiano wakati huu ambapo serikali inaanzisha kongani hizi, kujitokeza kutumia mbegu bora ili kutoa mazao yenye ubora ambapo pamoja na kongani za Dakawa kuna Mradi wa Mkualazi kwa ajili ya uzalisha wa sukari ambao upo kwenye maandalizi.