**********************
Adeladius Makwega-DODOMA
Nilifika katika ofisini siku hiyo na kuendelea na kazi za siku, huku nikitekeleza majukumu hayo vizuri, kwa desturi ilikuwa nikifika hapo mapema, basi hufanya majukumu kadhaa ya asubuhi ikiwamo vikao na kuyaweka vizuri mambo yote ikiwamo kuwasikiliza wageni kadhaa waliokuja mapema kupata huduma.
Majukumu hayo yalifanyika hadi saa tatu ya asubuhi, baada ya hapo ilikuwa ni wasaa na kufunga safari vijijini.
Kweli ilipofika saa tatu kamili tulianza safari ya kwenda kijijini ya kukagua miradi kadhaa iliyokuwa ikiendelea kwa wakati huo, mingi ilikuwa kwa ustawi wa maisha ya binadamu, ikiwamo Afya, Elimu, Kilimo na Mifugo.
Tulipomaliza hayo ilikuwa saa saba kamili tukaanza safari ya kurudi mjini na sasa nane juu ya alama tulifika mjini na kuendelea na kazi ya siku hiyo kwa karibu saa moja na nusu ambayo ilisalia kuimaliza siku hiyo kwa muda wa kazi.
Hapo ofisini nilikutana na watu kadha wakiningoja. Nilizungumza na mmoja baada ya mwingine na mgeni wa mwisho alikuwa binti mmoja.
Binti huyu alipoingia zililetwa kumbukumbu zake na kubaini kuwa alikuwa mwalimu katika shule moja ya sekondari iliyokuwa umbali mrefu na mji ule. Nilibaini kuwa alikuwa mwalimu pekee anayefundisha masomo ya Bailojia na Kemia katika shule hii. Pia nilibaini alikuwa na umri miaka 24 wakati huo.
Mwalimu huyu alikuwa dada mmoja mrembo, maji ya kunde, aliyevalia gauni ya rangi ya bluu iliyochanganyika na nyekundu (Zambarau), gauni hilo likiwa limemtosha vizuri, likisindikizwa na viatu vya kawaida visivyo na visigino virefu, kichwani akijifunga kilemba.
Nilimsikiliza mwalimu huyo ambaye aliomba likizo bila ya malipo ili aweze kwenda kusomea utawa.
Nilimsikiliza mwalimu huyu kwa umakini mno huku kabla ya kumkubalia ombi hilo na mimi nikimuomba jambo kuwa huo ulikuwa ni mwezi wa saba kidato cha pili na cha nne wakiwa katika maandalizi ya mitihani yao je atawezaje tena kuwaacha wanafunzi wale bila ya mwalimu wa masomo hayo?
“Mwalimu nakuomba usiondoke kwenda huko mafunzoni utawani kwa sasa, naomba jitahidi kuwafundisha vijana wetu hadi pale watakapomaliza mihutasari, ili uende huko masomoni utawani.”
Alitoka nje na kuwasiliana na kiongozi wa shirika lake na wakakubaliana juu ya jambo hilo alafu alirudi ndani nakuniambia sawa.
Muda huo huo niliipitisha barua yake ya ruhusa ya likizo ya bila malipo na yeye kuungama kuwa hadi Oktoba atakuwa amemaliza mihtasari ya kwa kidato cha pili na cha nne. Huku barua hiyo ikitumwa ngazi za juu na kushughulikiwa na wakuu wa shirika lake analokwenda kujiunga wakifuatilia hilo.
Mwalimu huyo alirudi kituoni kwake kuendelea na kazi akitekeleza yale makubaliano ili kuwasaidia wanafunzi wale waliokuwa hawana mwalimu mwingine wa masomo yale.
Kibinadamu nilijiuliza maswali mengi juu ya mwalimu huyu lakini ndiyo anaondoka katika taasisi hii na anakwenda kuwa mtawa.
Nilijaribu kuuliza katika shule yake, kwanza Mwalimu Mkuu na Mratibu Elimu Kata walimzungumzia kuwa ni mwalimu mchapa kazi anayewapenda wanafunzi wake vizuri mno.Nilimuuliza pia mwalimu mmoja wa shule ya msingi jirani ambaye niliwahi kusoma naye zamani Jijini Dar es Salaam alimzungumzia vizuri mno mwalimu huyu.
Wanafunzi walisoma na wakafanya mitihani yao vizuri huku mwalimu huyo akisimamia mitihani hiyo. Muda ulipofika alinitafuta na kuniaga na kuondoka zake kuelekea huko Iringa katika mafunzo hayo ya utawa.
Mwaka huo ulipita na kuanza mwaka mpya na baaada ya miezi kadhaa matokeo ya kidato cha nne yakatangazwa. Kwa kuwa nilikumbuka tukio la mwalimu huyu niliyafuatilia matokeo ya kidato cha nne ya shule hii hasa matokeo ya masomo ya Kemia na Bailojia, japokuwa shule hii ilikuwa katika mazingira magumu wanafunzi 29 walipata alama za ufaulu kwa somo la Kemia na wanafunzi 47 walifaulu somo la Bailojia. Katika shule yenye wanafunzi 39 waliofanya mtihani wa somo la Kemia na wanafunzi 62 waliofanya mtihani wa Bailojia.
Mara nyingi kwa umri wangu nilishuhudia watu wengi wakiingia utawa wakiwa na umri mdogo pengine wakiwa darasa la saba au wanapomaliza kidato cha nne. Lakini huyu aliingia utawa akiwa tayari ni mtumishi.
Kwani kitendo cha mwalimu bora huyu kukubali ombi langu la kurudi kituoni kwake kumalizia muhtasari ya masomo yake kwa wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne kilinipa picha juu ya imani ya mtumishi huyu kwani alikuwa mwema kwa binadamu wenzake.
Kwa siku ya leo nimemkumbuka mwalimu huyu, sifahamu yu wapi? kama alimaliza mafunzo yake na sasa yu mtawa au la. Sasa ni miaka kati ya 4-5 tangu tukio hilo litokee pengeni hata wale wanafunzi wake aliwafundisha kidato cha nne sasa wapo Chuo Kikuu kama si mwaka wa pili au watatu.
Kama tayari ameshakuwa mtawa au la binafsi namtakia maisha mema lakini ningetamani mno siku anayoweka nadhiri yake ya mwisho ya daima niwepo nishuhudie tukio hilo.
Namtakia maisha mema popote alipo mwalimu mrembo na hodari aliyeingia utawa.