Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na Viongozi wa Mkoa Shinyanga, Wadau pamoja na Watoto wenye Ulemavu alipotembelea Kituo cha Watoto wenye Ulemavu kilichopo Shule ya Msingi Bwagira kwa lengo la kutoa msaada kwa Wahitaji mbalimbali ambapo Ofisi yake imeshirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na Wadau ikiwa ni sehemu ya maadhimisho kuelekea Siku ya Wanawake.
Sehemu ya Watoto wenye Ulemavu wakisikiliza kwa makini maelezo ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi (Mb) alipowatembelea kwenye kituo hicho Macchi 6, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akieleza jambo walipotembelea Kituo cha Watoto wenye Ulemavu kilichopo Shule ya Msingi Bwagira kwa lengo la kutoa msaada kwa Wahitaji mbalimbali ambapo Ofisi yake imeshirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo pamoja na Wadau ikiwa ni sehemu ya maadhimisho kuelekea Siku ya Wanawake. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanawake kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Wanakikundi cha Wanawake Laki Moja walipotembelea Kituo cha Agape kinacholea Wahanga wa Ndoa na Mimba za Utotoni kwa lengo la kutoa mahitaji mbalimbali.
………………………………………………………………..
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu hassan imeendelea kutoa kipaumbele kwa Watu wenye Ulemavu kwa lengo la kukuza ustawi wa kundi hilo.
Amebainisha hayo Machi 6, 2022 walipotembelea Kituo cha Watoto wenye Ulemavu kilichopo Shule ya Msingi Bwagira kwa lengo la kutoa msaada kwa Wahitaji mbalimbali ambapo Ofisi yake imeshirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na Wadau ikiwa ni sehemu ya maadhimisho kuelekea Siku ya Wanawake.
Naibu Waziri Katambi alieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Miongozo na Mikataba ya Kimataifa ili kuifanya jamii itambue umuhimu wa kuwahudumia Watu wenye Ulemavu sambamba na kutoa kipaumbele kwa kundi hilo katika nyanja mbalimbali.
“Serikali imeendelea kutunga Sheria, kuandaa miongozo na taratibu ili kuwezesha Watu wenye Ulemavu waweze kupata haki na stahiki za msingi ikiwemo elimu, huduma za kiafya, ushiriki katika masuala ya uchumi pamoja na kushirikishwa kwenye maeneo ambayo wao watajiona ni sehemu ya ujenzi wa Taifa lao,” alieleza Katambi
Aliongeza kuwa, Serikali hii inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa Watu wenye Ulemavu na ndio maana imeweka Wizara maalum ambayo inashughulikia masuala yao kwa ukaribu.
“Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan anawajali na kuwapenda sana wenzetu wenye Ulemavu, Vijana, Watoto, Wanawake na amekuwa akipaza sauti kwa ajili ya kupigania haki za makundi hayo,” alisema Naibu Waziri Katambi
Sambamba na hayo, Naibu Waziri Katambi alipongeza jitihada za Wanawake katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo mbalimbali kwa namna wanavyojitoa katika jamii zinazowazunguka na kusaidia watu wenye uhitaji.
“Kwa kweli jambo hili ni kubwa na nitaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana pamoja nanyi ili kuhakikisha wenye mahitaji wanapata haki zao,” alisema
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko alitumia fursa hiyo kumshukuru Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi kwa namna alivyojitoa kushirikiana na Wanawake wa Mkoa huo.
Pia, alieleza kuwa kuelekea Siku ya Wanawake Duniani ambayo uadhimishwa Machi 8 kila mwaka, katika wilaya hiyo ya Shinyanga mjini wanawake waliona umuhimu wa kujitoa ili waweze kusaidia wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali mkoani hapo, hivyo aliwashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa namna walivyojitoa kutoa michango yao katika kusaidia ufanikishaji wa tukio hilo muhimu.
Naye mmoja wa wanufaika wa mahitaji hayo, Vediana Wilson alitoa shukrani kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Kikundi cha Wanawake Laki Moja pamoja na wadau mbalimbali kwa namna wanavyojitoa kusaidia watu wenye uhitaji.
Wakati wa zoezi hilo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Kikundi cha Wanawake Laki Moja pamoja na wadau mbalimbali walitembelea pia Gereza la Wanawake la Matanda, Kituo cha Agape kinacholea Wahanga wa Ndoa na Mimba za Utotoni.