Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo (wapili kutoka kushoto) akipewa ufafanuzi na Mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kituo cha kufua umeme kwa kutumia gesi asilia vya Ubungo 1 (Ubungo Gas Plant 1) kilichopo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba (wa kwanza kutoka kulia), Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa tatu kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, maofisa kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO wakati wakikagua mitambo ya umeme katika kituo cha Kinyerezi ll ili kujionea utendaji kazi wa mitambo hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Maharage Chande akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kumaliza kukagua wa mitambo ya umeme katika kituo cha Kinyerezi II.
Muonekano wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia iliyopo Ubungo 1 (Ubungo Gas Plant 1) na Kinyerezi ll jijini Dar es Salaam.
*************************
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imefurahishwa na utendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kuwatumia mafundi wawaza katika kufanya ukarabati wa mitambo pamoja na kuongeza jitiada za upatikanaji wa umeme wa kutosha.
Hatua hiyo imekuja baada ya leo Mach 6 mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kufanya ziara ya kutembelea mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme katika vituo vya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia vya Ubungo 1 (Ubungo Gas Plant 1) na Kinyerezi ll ili kujionea utendaji kazi wa mitambo hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mitambo ya uzalishaji umeme, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo, amesema kuwa TANESCO wanafanya kazi kubwa ili kuhakikisha waondoa changamoto ya ukosefu wa umeme hapa nchini.
Mhe. Sillo ni Mbunge Jimbo la Babati, amesema kuwa kituo cha umeme Ubungo 1 wamewakuta mafundi wazawa wakikarabati mitambo ya uzalishaji umeme jambo ambalo ni rafiki, huku akieleza kuwa ukarabati wa mitambo ya Ubungo 1 ukikamilika, hali ya upatikanaji umeme itaimarika zaidi ya ilivyo hivi sasa.
“Kwa bahati nzuri, TANESCO hawajalalamika kuhusu bajeti, na kwa mwaka 2021/2022 tumeitengea Wizara ya Nishati kiasi cha shilingi trilioni 2.3, tuna amini bajeti iko vizuri” amesema Bw. Sillo.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema kuwa uwekezaji uliopo hivi sasa ndani ya TANESCO ni mkubwa, lakini uwekezaji zaidi unahitajika kutokana na kuzidi kuongezeka mahitaji ya umeme kila siku.
“Uwekezaji huu naweza kusema haujatosha kwa kuwa mahitaji ya umeme bado ni makubwa na yanaongezeka, miundombinu ya umeme inahitajika kukua zaidi na uwekezaji uendelee kuongezeka” amesema Mhe. Byabato
Naibu Waziri Mhe. Byabato ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya uwekezaji katika Wizara ya Nishati, ili kuzalisha umeme wa kutosha kwa ajili ya wananchi, umeme ambao utakuwa wa gharama nafuu na unaotabirika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Maharage Chande amefafanua kuwa shirika hilo linafanya kazi ya maboresho na ukarabati na unafuu mkubwa unaendelea kupatikana kwa wateja.
Amesema kuwa malalamiko ya wateja yamepungua, huku akisisitiza kuwa bado wako kazini kuhakikisha kwamba changamoto zote kwa zinaisha.
Bw. Chande amebainisha kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu wataanza kutumia mita janja (smart meter), ambapo wafanyakazi ya TANESCO wakiwa ofisini wanaona matumizi ya mteja.
“Tunaweza kuona matumizi yako, tunaweza kuwasha na kuzima umeme, mwezi Julai tutaona mita janja zinaanza kuingia, na hivyo mita za zamani tutazibadilisha” amesema Bw. Chande.
Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wameshiriki watendaji mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja na maofisa kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.