*********************
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
DIWANI viti maalum, Kibaha Mjini Lidya Mgaya amejitolea kujenga nyumba ya watoto yatima wanne ,na Bibi yao wa miaka 80 ambao maisha yao yanaendeshwa na kaka yao ambae amefeli kidato cha nne kwa kuelekeza akili kusaidia familia hiyo.
Lidya anajenga nyumba hiyo huko kata ya Bamba , Kongowe ambapo anashirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha lengo lake.
Akiwa katika eneo la ujenzi Lidya alisema Faida Hamis Ramadhani, Mohamed Hamis Ramadhani, Selemani Hamis Ramadhani na, Sofia ni ndugu ambao wazazi wao wamefariki na kubaki na bibi mzaa mama yao ambae nae ni kikongwe.
Diwani huyo alieleza, Faida Hamis Ramadhani huyu alikua akisoma Kibaha girls na alipata bahati ya kusomeshwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini,Silvestry Koka, lakini masomo yake yalikatishwa na ujauzito akiwa shuleni kwa wakati ule elimu ilikua ya kulipia.
“Iliniuma,maisha ya huyu mtoto,niliwaza Maisha yangu niliyoyapitia, natamani kuona mtoto wa kike akisoma na kujiendeleza kimaisha, Sasa huyu mtoto ni mama lishe, kaka ndio abangaize wale , kiukweli niliona niwajengee ili watoke katika kijumba ya tope waishi japo eneo bora zaidi”alisema Lidya.
Pia alieleza, wakazi wa Bamba walimuomba asaidie watoto hao wakati yeye alipokuwa kwenye kampeni ya LIDYA KAZINI ,kukandika na kuboresha nyumba Saba za waasisi wa Chama CCM ,huko Kongowe na akakubali.
“Hadi sasa nyumba imepanda kozi tatu juu ya linta,Bado bati 50 mbao za kuezekea 4 by 2=45 na 2 by 2 = 45,
Milango 5 ,geti moja dogo madirisha matatu makubwa dogo moja, saruji mifuko 18 kwa ajili ya lipu , shimo la choo na choo cha nje ,maji kuvuta na umeme.”alifafanua Lidya.
Aliwaomba wafadhili na wadau wa maendeleo ya jamii kujitokeza kushirikiana nae katika suala hilo,kwani yeye ameguswa anahitaji kuungwa mkono.
Nae Mohamedi Hamic Ramadhani alisema amemaliza form four mwaka jana ila amefeli kwa sababu ya kusaidia wadogo zake kuhusu chakula.
“Seleman yeye ana miaka 14 darasa la sita ,Sophia miaka saba darasa la pili hawa ni wadogo, inabidi niwaangalie, ilinibidi niongeze nguvu ya kupigania maisha japo ya kula ya wadogo zangu kumbe ndio nashuka kitaaluma kimasomo nikafeli”alisema kwa uchungu Mohamedi.
Inadaiwa kwamba ,tamu na raha ya maisha ilipotea wakati wazazi wao walipofariki na kujikuta ndugu wa upande wa ubabani wakiwa wafukuza katika nyumba waliyokuwa wakiishi ndipo wakapata wazo la kwenda kwa bibi yao ambae nae alikuwa analelewa na baadhi ya ndugu wa umamani kwao ,ambapo nako baada ya kuona Bibi kakubalj wajukuu zake maisha yalivyo magumu nae ..safari yake ya kusaidiwa iliishia hapo .
Ndipo walipoanza maisha mapya ya kusaidiwa na majirani wa kata ya Bamba huku wakiishi kwenye nyumba ya udongo kuendesha maisha Yao.