NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
WANAFUNZI 13 katika jimbo la Chalinze ,Mkoani Pwani wamepata mimba kwa kipindi cha miezi nane kuanzia Jan -agost mwaka huu,ambapo wanafunzi 12 kati ya hao ni kata ya Msata.
Kutokana na idadi hiyo ,madiwani wa halmashauri ya Chalinze pamoja na mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete wamelaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wanaume kutia wanafunzi mimba za utotoni hali inayosababisha kukatisha masomo yao.
Akizungumza wakati wa baraza la madiwani katika taarifa za kata kwa kata, Ridhiwani alisikitishwa na namba hiyo na kudai ni kubwa kwa kipindi kifupi.
Alisema ,shule ya sekondari Msata imekuwa ya mwisho ,wanafunzi wamezidi utoro na mimba zimeshafika tisa suala ambalo si jema na halifurahishi.
“Kesi ya jinai haifi, haiozi ,haipotei ,kutembea na binti wa miaka 18, hata ikifika mwaka 2060 ndipo ukagundulika ulimpa mimba mwanafunzi 2019 ,sheria bado ina meno utakamatwa “alifafanua Ridhiwani.
Ridhiwani alibainisha kuwa ,polisi isimamie kesi hizo kwa kutoa haki na sheria ichukue mkondo wake.
Nae OCS WAMI ,Joseph Ogutu alitaka ushirikiano dhidi ya kesi hizo.
Aliomba jamii kishirikiana na polisi ,kwakuwa kuna changamoto ya wazazi kwenda kudokeza wahusika na kusababisha kukimbia.
Ogutu alieleza ,kati ya kesi hizo 13 ,wamekamatwa watuhumiwa watatu pekee hadi sasa .
Awali akisoma taarifa ya kata kwenye baraza la madiwani, Diwani wa viti maalum Msata na mwenyekiti wa kamati ya elimu,afya na maji Chalinze,Rehema Mno alisema kati ya wanafunzi hao 13 ,wanafunzi tisa ni wa sekondari na wanne ni wa msingi.
Alisema ,suala hilo linaumiza kwani wakati serikali ikipiga vita vitendo hivyo kumbe bado kuna maeneo wanaendelea kukatisha ndoto za wanafunzi wa kike.
Rehema alieleza ,wazazi na walezi wanachangia kukua kwa suala la mimba za utotoni kwakuwa wanaficha wahusika waliowapa mimba watoto wao na wakati mwingine wanakaa nao kuyamaliza mezani.
“Watuhumiwa wanakimbia ,tumejipangia mkakati kwamba watoto wakipelekwa kupimwa madaktari wasitoe majibu kwanza hadi watakapowaruhusu ndipo waende moja kwa moja polisi kuwataja wahusika na kwa kufanya hivyo watakamatwa kirahisi ,”
“Wakirudi majumbani watatoa siri na hapo ndipo watuhumiwa wanapokimbia”alifafanua Rehema.
Mtendaji wa kata ya Msata, Balthazary Miti ,alisema katika kata hiyo mimba ni 12 ,kati ya hizo tisa ni shule ya sekondari.