Na.Alex Sonna,DODOMA
VINARA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Timu ya Yanga wameendeleza vichapo kwa wapinzani baada ya kuizamisha mabao 3-0 Kagera Sugar kutoka Mkoani Kagera mchezo wa mzunguko wa 16 uliochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikicheza kwa kushambualiana kutokana na wachezaji kuonyesha ufundi wa hali ya juu.
Mshambuliaji hatari kwa sasa Fiston Mayele aliwanyanyua mashabiki wa Yanga dakika ya 30 akifunga bao kwa kichwa baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Saido Ntibazonkiza.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko hata hivyo mabadiliko hayo yamewasaidia Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Mayele alirudi tena kambani dakika ya 50 akifunga bao safi kwa kichwa kutoka kwa Saido Ntibazonkiza ambaye kwa leo amekuwa hatari kwa wapinzani na dakika ya 64 Saido Ntibazonkiza alipigilia msumari wa tatu akimalizia pasi ya Fiston Mayele.
Kwa ushindi huu Yanga wameendelea kujichimbia kileleni kwa kufikisha pointi 42 huku Fiston Mayele akifikisha mabao 9 akizidiwa moja na Reliants Lusanjo wa Namungo mwenye mabao 10 na Kagera Sugar wanabaki nafasi yao ya nane wakiwa na Pointi 20.
Matokeo mengine Ruvu Shooting imeshindwa kutamba uwanja wake baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Dodoma jiji katika uwanja wa Sokoine Mbeya Tanzania Prisons na Mbeya City wametoka sare ya kufungana bao 1-1.