Mkuu wa Ukaguzi Kitengo cha Bandarini kutoka Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) Muhammed Shadhil Shauri, akitoa Maelezo kuhusu kuteketezwa kwa Mchele aina ya Al-faiz uliyoingia maji ya bahari wakati wa kusafirishwa, Kontena moja Tani 27, mali ya Kampuni ya Al-faiz General Store, huko Jaa Kuu la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya Mchele aina ya Al-faiz uliyoingia maji ya bahari wakati wa kusafirishwa, Kontena moja Tani 27, mali ya Kampuni ya Al-faiz General Store, Ukimwaga kwa ajili ya kuteketezwa na Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) , huko Jaa Kuu la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
Gari aina ya Kijiko likisaga Mchele aina ya Al-faiz uliyoingia maji ya bahari wakati wa kusafirishwa, Kontena moja Tani 27, mali ya Kampuni ya Al-faiz General Store, kwa lengo la kuteketeza na Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) , huko Jaa Kuu la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya Mchele aina ya Al-faiz uliyoingia maji ya bahari wakati wa kusafirishwa, Kontena moja Tani 27, mali ya Kampuni ya Al-faiz General Store, Uliyomwaga kwa ajili ya kuteketezwa, Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) huko Jaa Kuu la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.
(PICHA NA MARYAM KIDIKO – MAELEZO ZANZIBAR)
…………………………………………………
Na Maryam Kidiko- Maelezo Zanzibar
Jumla ya Tani 27 za Mchele zimeteketezwa na Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) baada ya kubainika kuwa mchele huo haufai kwa matumizi ya binadam.
Shughuli ya uteketezwaji imefanyika Jaa kuu la Kibele Mkoa wa Kusini Unguja chini ya usimamizi wa Maafisa wa ZFDA.
Akizungumza na Wanahabari mara baada ya uteketezaji Mkuu wa Ukaguzi kitengo cha Bandarini Mohammed Shadhil Shauri amesema, Mchele huo uliharibika baada ya Kontena lililoubebea kuingia maji ya chumvi wakati wa kusafirishwa.
Amesema kuwa Mchele huo uliingizwa bandarini mwishoni mwa Mwezi Januari mwaka huu na Kampuni ya Al-faiz General Store ukitokea nchini Pakistan.
Shauri amefafanua kuwa Kampuni hiyo iliingiza jumla ya Makontena 10 ambapo moja ya Makontena hayo liliharibika na kupelekea Mchele huo kuingia maji ya chumvi.
“Tulivyoyakagua Makontena yote 10 tukagundua Kontena moja Mchele umeingia maji na haufai tena kwa matumizi ” alisema Shauri.
Amesema baada ya kubaini tatizo hilo hatua iliyofuata ni kuuteketeza ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa watumiaji.
Shauri ametoa wito kwa Wafanyabiashara kufanya utafiti wa kutosha kwa Makampuni wanayonunulia bidhaa sambamba na Makontena ya usafirishaji ili kuepuka kuingia hasara.
Akielezea hali halisi ya uingizwaji wa biashara kutoka nje ya nchi Shauri amesema kwa sasa wafanyabiashara wengi wamepata uelewa na hivyo kupelekea kupungua kwa wimbi la uingizwaji wa bidhaa mbovu.
Amesema kwa sasa inaweza kupita miezi mitano bila kuteketeza bidhaa yoyote kwa vile bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi vigezo vya ubora.
“Zamani kila baada ya muda tulilazimika kuteketeza Bidhaa mbovu zilizoingizwa nchini ila kwa sasa uelewa wa w
Wafanyabiashara umeongezeka na hivyo kupelekea kuingiza bidhaa zinazokidhi vigezo” alisema Shauri.
Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) umeundwa kwa lengo la kusimamia na kudhibiti bidhaa za Chakula, Dawa na Vipodozi ili kulinda afya za watumiaji wa bidhaa hizo nchini.