…………………………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
WANANCHI wilayani Nzega Mkoani Tabora wamepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 katika kuboresha miundombinu ya afya kwenye vituo vyote vya kutolea huduma hizo.
Wakizungumza hivi karibuni walielezea kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali kwa kupeleka fedha za kutosha katika wilaya hiyo ili kuongeza majengo ya hospitali ya wilaya, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.
William Luhemeleja mkazi wa Mtaa wa Nyasa, kata ya Nzega Mashariki alikiri kuwa huduma za afya katika hospitali ya wilaya na vituo vya afya zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.
Alibainisha kuwa sasa hivi mtu akienda hospitali anapata huduma zote za kitabibu ikiwemo dawa, watoa huduma pia wanapatikana muda wote na wamepunguza lugha mbaya kwa wagonjwa.
Diwani wa kata ya Ijanija na Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Nzega, Barabela Makono alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea fedha za kutosha ili kuboresha majengo ya hospitali, vituo vya afya na ununuzi wa vifaa.
‘Serikali ya awamu ya sita imewatendea haki wananchi, imetujengea hospitali nzuri ya wilaya, vituo vya afya na maboma ya zahanati yaliyokuwepo katika vijiji mbalimbali yamekamilishwa, hili ni jambo la kujivunia sana,’ alisema.
Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo Jabil Juma aliishukuru serikali kwa kuwaletea fedha kiasi cha sh mil 650 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Alifafanua kuwa sh mil 300 za UVIKO-19 ni kwa ajili ya ujenzi jengo la huduma za dharura (EMD) katika hospitali ya wilaya, sh mil 250 za tozo kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) kwenye Kituo cha Afya cha kata ya Mwanzori na sh mil 100 za umaliziaji ujenzi wa zahanati ya Itilo na Idalo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Shomari Mndolwa alisema kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati kuboresha maisha ya wananchi katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, barabara na maji.
Alibainisha kuwa maboresho makubwa ya miundombinu ya afya yamechochea kwa kiasi kikubwa utoaji huduma bora kwa jamii, hivyo akawataka kutunza vizuri miundombinu hiyo ili idumu na kunufaisha wananchi wengi zaidi.
Mwisho.
Pichani…Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera Bulimba (aliyesimama) akiongea na watumishi wakiwemo watendaji wa kata wa halmashauri ya Nzega Mji hivi karibuni mjini humo, kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Shomari Mndolwa (mwenye suti nyeusi). Picha na Allan Ntana.