Mkurugenzi wa Amana Benki Dkt.Muhsin Masoud akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya Halal Pesa uliofanyika jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za M-Pesa Vodacom, Tulisindo Rashid akizungumza huduma hiyo ya Halal Pesa itakavyofanya kazi
Mkuu wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa M-Pesa, Polycarp Ndekana, akizungumza katika uzinduzi wa halal pesa uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
****************
BENKI ya Amana kwa kushirikiana na Mtandao wa simu za mkononi wa Vodacom wamezindua huduma mpya ijulikanayo kama ”Halal Pesa”.
Huduma hiyo mpya sasa itapatikana kwa wateja wa Vodacom wanaotumia M-Pesa na wale wa Amana Bank kwa kuzingatia misngi ya sheria ya kiislamu.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Masoud, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifikiria jinsi ya kuwafikia wateja wengi zaidi ambao wanapenda kutumia miamala ya kifedha kwa mujibu wa sheria ya kiislamu.
Dkt. Masoud alisema Amana Bank imekuwa ikibuni njia mbalimbali za kuwafikia wateja wake wazamani na wapya hivyo wameweza kuanzisha huduma hiyo ya halal pesa ambapo wateja wa Vodacom wanaotumia M-pesa wataipata huduma hiyo mpya inayozingatia misingi ya sheria ya kiislamu.
Alisema katika huduma ya halal pesa mteja wa Amana Bank anaweza kufanya miamala yake kwa kutumia Vodacom M-Pesa huku akiwa bado yupo kwenye sheria za uislamu kuhusu miamala ya kifedha.
Dkt. Masoud alisema Amana Bank imetimiza miaka nane ikiendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria za kiislamu.
Alisema Benki hiyo ndio benki pekee hapa Tanzania ambayo mfumo wake wa kifedha umesimamia sheria za benki za kiislamu.
Hata hivyo alisema licha ya Benki hiyo kufuata sheria za kiislamu katika uendeshaji wake, bado inaendelea kuwahudumia wateja wake bila ya kubagua dini, rangi wala kabila hivyo amewataka wateja wao kutambua kuwa Benki hiyo ipo kwaajili ya kila mtu.
Alisema kuanzishwa kwa huduma ya halal pesa kwa kushirikiana na mtandao wa simu wa Vodacom kutasaidia watu wengi zaidi kufikiwa na huduma giyo ambayo inafuata sheria za kiislamu.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha huduma za M-Pesa kutoka Vodacom, Tulisindo Rashid alisema, halal pesa imelenga zaidi ya robo tatu ya waislamu nchini Tanzania ambao kwa kupitia mfumo wa M-Pesa wataweza kuweka fedha na kupata faida kihalali (bila ya riba).
Alisema kwa muda mrefu waislamu wamekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za kuweka fedha zinazfuata sheria za dini ya kiislamu ambapo huduma hiyo itawezesha watumiaji wake kuweka fedha kwa njia rasmi ya halal pesa.
Alisema Vodacom itaendelea kutoa ufumbuzi wa mambo mbalimbli ili kukidhi mahitaji ya wateja wake katika mfumo wa kifedha kwa kutumia teknolojia ya kidigitali yenye gharama nafuu na uwezo wa hali ya juu.
Aliongeza kwa kusema, halal pesa ni huduma rahisi na ya kipekee inayoendana na sheria za kiislamu ambayo imegawanyika katika mafungu mbalimbali.
Alifafanuwa mafungu hayo ni pamoja na kuweka pesa binafsi, kwaajili ya kwenda hija, watoto au kuweka pesa kwa muda mrefu kuanzia miezi 3 hadi 12.
Aidha, alitoa wito kwa maimamu wa misikiti kufungua Akaunti kupitia halal pesa ambapo msikiti utapewa namba maalum ya utambulisho (Code number) itakayowawezesha waumini kuchangia michango ya msikiti hata kama hawapo msikitini.
Alisisitiza kuwa, huduma hiyo ni salama na kwamba inafuata misingi ya kiislamu kwa kupata muongozo kutoka kwa wanazuoni wa kiislamu kuhusu masuala ya kifedha.
Sheria ya kiislamu imeharamisha riba na kuhalalisha biashara hivyo muislamu anapofanya miamala ya kifedha huchunga mipaka ya kisheria na kujiepusha na riba.
Kwa huduma hii mpya ya halal pesa iliyozinduliwa kwa ushirikiano wa Amana Bank na Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom itamuwezesha muislamu kuweka fedha Amana Bank na kuzitoa kwenye M-Pesa huku akiwa hakutani na riba na badala yake atapata gawio la faida ambalo limeruhusiwa katika sheria ya uislamu.