Meneja wa Shamba la Miti Wino lililopo kata ya Wino Halmashauri ya Madaba linalomilikiwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Glory Kasmir kulia,akimueleza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge hatua inayoendelea ya kupanda miti katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na shughuli za kibidamu katika mkoa huo wakati wa uzinduzi wa mpango wa upandaji miti kimkoa uliofanyika katika kata ya Mateteleka.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kushoto,akizungumza na Diwani wa kata ya Mateteleka Halmashauri ya Madaba Humphrey Mwenda na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Olaph Pili katika kuhusu uharibu wa mazingira na vyanzo vya maji kutokana na shughuli mbalimbali za kibidamu katika kata hiyo.
Na Muhidin Amri,Madaba
………………………………………………………….
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,ameagiza wakala wa huduma za Misitu Tanzania(TFS)kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kuongeza kasi ya kupanda miti katika maeneo ya wazi yaliyoathiriwa na shughuli za kibinadamu katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Ibuge ametoa agizo hilo jana, wakati akizundua mpango wa upandaji miti kimkoa uliofanyika katika kijiji cha Mwande kata ya Mateteleka Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.
Aidha Brigedia Ibuge,amewaonya wananchi kuacha tabia mbaya ya kuchoma kwa makusudi miti inayopandwa na Serikali kupitia wakala wa huduma za misitu(TFS)kwa kuwa hiyo ni sehemu ya miradi inayoliingizia Taifa fedha nyingi.
Alisema,kuchoma moto kwa makusudi mashamba ya miti ni ushamba na kamwe Serikali haitawavumilia hata kidogo watu hao kwa sababu Serikali inatumia fedha nyingi kuandaa mashamba hayo na amewataka wananchi, kuheshimu uwekezaji huo.
Katika hatua nyingine,Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza TFS kwa kupanda miti laki saba tangu mvua za masika zilipoanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Hata hivyo, ameomba kazi hiyo iwashirikishe wananchi na kutoa ushauri kuhusu miti sahihi inayopaswa kupandwa, badala ya kuacha wananchi wanapanda miti holela na matokeo yake kukauka kutokana na kupandwa sehemu zisizo sahihi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa,Serikali haiwezi kutekeleza kila jambo pekee yake, bali wananchi ni muhimu washirikishwe na washiriki katika shughuli zote za maendeleo kwani hatua hiyo itasaidia kulinda miradi hiyo kwa kuwa wataiona ni yao.
Akizungumza na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Madaba wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Olaph Pili Mkuu huyo wa mkoa alisema, maeneo mengi ya Madaba yana changamoto ya ukataji na uchomaji moto miti,hivyo ni lazima kupanda miti kwa wingi.
Mkuu wa mkoa ameitaka Halmashauri ya Madaba, kutunga na kutumia sheria ndogo zinazomtaka kila mwananchi katika eneo lake kuhakikisha anapanda miti na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaofanya shughuli kwenye vyanzo vya maji na maeneo yasioruhusiwa.
Kuhusu wananchi waliotoa maeneo yao ya kilimo na kuwekwa mipaka (Bikoni) alisema, ni vyema Halmashauri kufanya tathimini ya kina kujua watu wangapi walioathirika ili wapewa maeneo mengine kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao.
Amewaonya wananchi walioondolewa katika maeneo ya hifadhi kufanya shughuli zao kutodai fidia yoyote kwani wao ndiyo wenye makosa kwa kuingia na kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vyanzo vya maji.
Kamanda wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini Manyisye Mpokigwa alisema,TFS ina jukumu la kuhakikisha vyanzo vyote vya maji vinalindwa kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwamo mamlaka na wakala za maji(Ruwasa) kwa kupanda miti katika maeneo yote yaliyoathirika na shughuli za kibinadamu.
Naye Meneja wa shamba la miti Wino Glory Kasmir alisema, hadi sasa wamefanikiwa kupanda miti laki saba katika vijiji na maeneo ya ofisi za Serikali kwa ajili ya kurudisha maeneo yaliyoathirika katika hali yake ya asili.