Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi Akizugumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya UVIKO 19 kwa wadau wa Sekta ya Utalii yaliyofanyika Februari 21,2022 Katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Manispaa Mji wa Songea.
Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki akizungumza alipokuwa akifungua rasmi mafunzo hayo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Dkt. Naiman Mbise Mratibu wa Mradi wa Mradi Mafunzo kwa watoa huduma katika mnyororo wa Sekta ya Utalii nchini chini ya Mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, akizungumza wakati wa ufunguzi huo.
Mratibu wa Mafunzo hayo Mkoa wa Ruvuma Elina Makanja akizumzia jinsi walivyojipanga Katika kutoa mafunzo hayo Mkoani humo.
Wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii Mkoa wa Ruvuma wakifuatilia hotuba mbalimbali za ufunguzi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi (wa kwanza Kushoto aliyekaa), katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki (Katikati) na Mratibu wa Mafunzo hayo Mkoa wa Ruvuma Elina Makanja wakiwa kwenye Picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii.
Na: Mwandishi wetu, SONGEA.
Chuo cha Taifa cha Utalii kimezindua mafunzo ya siku tano ya UVIKO 19 kwa wadau zaidi ya 140 waliopo kwenye mnyororo wa huduma za utalii katika Mkoa wa Ruvuma ili kuwajengea uwezo wa namna ya kujikinga katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wakati wanapotoa huduma kwa wageni pindi wanapotembelea maeneo yao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Februari 21,2022 Katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Mji wa Songea Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi Sedoyeka amesema kuwa Mafunzo hao yamefadhiliwa na MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAKABILIANO DHIDI YA UVIKO 19 kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dkt. Sedoyeka amesema kuwa Chuo kimeamua kutoa mafunzo hayo kwa wadau wa utoaji wa huduma za Utalii baada ya kubaini kuwa baadhi yao walikuwa bado hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na Uviko 19 pindi wanapowahudumia watalii .
Amesema kuwa Chuo kinatoa mafunzo hayo kwa wadau muhimu katika mnyororo wa utalii ili wadau hao waweze kuboresha huduma zao na thamani ya pesa inayotolewa na mgeni au mtalii kuonekana. chuo kinatoa mafunzo hayo kwa watoa huduma hao kwa kuwa wengi wao hawana weledi wa utoaji huduma hasa wakati huu wa janga la UVIKO-19 ili kujikinga wao wenyewe pamoja na wageni wanaopata huduma zao.
Aidha, Dkt. Sedoyeka amesema mafunzo haya kwa mkoa wa Ruvuma yamekuja wakati sahihi ambapo kuna shughuli mbalimbali za utalii wa makumbusho, kupanda milima, fukwe n.k lakini watoa huduma kutokuwa na uelewa mpana na wa kibunifu wa kutoa huduma hizo.
Pia amesema mafunzo yanatolewa katika mikoa nane ikijumuisha Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Mara na Mwanza. mbapo mpaka sasa mafunzo yamekamilika mkoa wa Lindi na Mtwara; yanaendelea mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa siku tano,na badae kufikia mikoa mingine minne.
Katika hatua nyingine Dkt. Sedoyeka amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zinawezesha kukabiliana na Uviko 19 kwenye jamii pamoja na kwamba mpango huo unanesha nia madhubiti ya Serikali ya awamu ya sita Katika kukabiliana na janga hilo.
Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa huo Brigedia Wilbert Ibuge kwenye uzinduzi huo katika nafasi ya mgeni rasmi amesema kuwa sekta ya utalii imekuwa ikitoa fursa mbalimbali ikiwemo suala la ajira hivyo inatakiwa kuizingatia kikamilifu .
Ndaki amesema kuwa katika kipindi cha janga kubwa la Corona utalii uliyumba katika Nchi mbalimbali hivyo kwa sasa inatakiwa kuitumia elimu ya Uviko 19 ipasavyo ili kulinda watalii na jamii kwa ujumla .
Naye Maajabu Mbogo Afisa Utalii katika pori la Limbaramba ambaye ni mmojawa washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo hayo yataleta neema ya kuongezeka kwa watalii na kuifanya Serikali iweze kupata mapato kupitia watalii hao.
Hata hivyo Mbogo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka fedha za Uviko19 katika Sekta hiyo na kwamba RAIS ameangalia maslahi mapana ya nchi hasa katika kuikomboa Sekta ya Utalii nchini ambao imeathirika na Jana hilo kwa kiasi kikubwa.
Katika mafunzo hayo jumla ya mada Sita zitatolewa na wakufunzi wakufunzi mbalimbali kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii na mafunzo hayo yatafikia kilele chake ijumaa Februari 25,2022.