……………………………………………………….
Na John Walter-Manyara
Madereva wa bodaboda mkoa wa Manyara wameiomba mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji (EWURA) kuvifungia vituo vya mafuta ambavyo vinatoa mafuta machafu na kusababisha vyombo vyao kuharibika na kushindwa kufany kazi vizuri.
Wameyasema hayo leo februari 21,2022 katika semina iliyoandaliwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa huduma za nishati na maji (EWURA CCC) Mkoa wa Manyara iliyolenga kutoa elimu juu ya haki na wajibu kwa watumiaji wa huuma za nishati na maji iliyofanyika mjini Babati.
Baadhi ya madereva wa pikipiki (Bodaboda) mjini Babati wakizungumza kwa nyakati tofauti na kituo hiki wamekiri kuuziwa mafuta machafu hali inayosababisha pikipiki zao kuzima wakiwa njiani.
Hata hivyo Madereva hao wameiomba mamlaka husika ione namna ya kudhibiti tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Boda boda mkoa wa Manyara Omari Adamu aliuliza “Kwa kuwa baadhi ya vituo vya mafuta kutoa huduma mbaya ya mafuta machafu, kwanini EWURA isione haja ya kuvifungia vituo hivyo” aliuliza mwenyekiti huyo bila kutaja kituo cha mafuta
Akizungumza katika semina hiyo mwezeshaji kutoka EWURA CCC Amina Mwanja amesema katika kudhibiti hilo, madereva wanapaswa kudai risiti mara baada ya kupata huduma ili kunapotokea shida ya aina hiyo iwe rahisi kushughulikiwa huku akiwashauri wasiwe wepesi wa kukubali kupewa huduma zisizo na ubora.