Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM,) Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Kate Kamba akizungumza katika mahafali ya Chuo cha Furahika Education College yaliyofanyika tarehe 18/02/2022 Jijini Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo cha Furahika Education College Bw.David Msuya akizungumza katika mahafali ya Chuo cha Furahika Education College yaliyofanyika tarehe 18/02/2022 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM,) Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Kate Kamba akizungumza jambo na Mkuu wa Chuo cha Furahika Education College Bw.David Msuya katika mahafali ya Chuo cha Furahika Education College yaliyofanyika tarehe 18/02/2022 Jijini Dar es Salaam.
Wahitimu wa Chuo cha Furahika Education College wakifurahi katika mahafali ya Chuo hicho yaliyofanyika tarehe 18/02/2022 Jijini Dar es Salaam
*********************
MWENYEKITI Wa Chama cha Mapinduzi(CCM,) Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Kate Kamba amewataka wanafunzi wa chuo cha Furahika Education College kuzingatia nidhamu na kujituma ili waweze kujijenga kiuchumi na kutimiza malengo yao.
Akizungumza katika mahafali ya tisa ya chuo hicho yaliyofanyika mwisho wa wiki Bi. Kate Kamba amesema chuo hicho kinaunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora itakayowakwamua kiuchumi.
Amesema, Maarifa yanayotolewa na chuo hicho ikiwemo mafunzo ya hoteli, ufundi na sanaa Yana fursa kubwa na kuwataka kujituma na kuzingatia nidhamu.
“Nimesikia hapa chuo kinawatafutia fursa za mafunzo, mkajitume na sio kutumwa…Nitakuwa mshirika wa chuo hiki katika kuhakikisha vijana wengi wanapata mafunzo haya.” Amesema.
Pia Bi. Kamba amesema katika kuboresha sekta ya elimu Serikali imetoa shilingi Trilioni 1.3 kwa ajili ya kujenga madarasa na kwa Mkoa wa Dar es Salaam madarasa 947 yamejengwa.
“Chuo hiki kipo chini ya VETA na mafunzo yanayotolewa yana tija kwa jamii, niwasihi mkuze sekta ya utalii ili ikifika 2025 tufikie lengo la kufikia milioni 10.” Amesema.
Aidha ametumia wasaa hao kuwataka wananchi kushiriki kwa karibu zaidi katika mchakato wa sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka huu nchini kote.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho David Msuya amesema, wanafunzi 23 wamehitimu mafunzo hayo katika kozi mbalimbali ikiwemo hoteli, ushonaji, sanaa, mapambo na muziki huku changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa taulo za kike na uhaba na ubovu wa kompyuta.
“Tunatoa mafunzo haya kwa wanafunzi wa kike waliofeli darasa la saba na walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali….Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kuwasaidia watoto wetu taulo za kike ili waweze kujisitiri wakati wa hedhi.” Amesema.
Chuo hicho kinatoa mafunzo ya ufundi bure kwa wanafunzi wakike walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali ili kuwajenga kiuchumi na kutimiza malengo yao.