*********************
Adeladius Makwega-DODOMA
Februari 18, 2022 nilitoka zangu madongo poromoka na kuelekea huko kwa pangu pakavu tia mchuzi. Nilipanda daladala kwa mwendo wa dakika 45 hivi na nakushuka njia kuelekea niendapo.
Hapa nilipanda bodaboda ya yule kijana wangu ambaye mara zote anibeba na mara nyingi nimekuwa nikikusimulia habari zake, kijana huyu alinisalimu huku akiwa amevalia koti lake la mvua, nilimuuliza kulikoni mbona jua linawaka na koti maungoni? Akisema kuwa hali ya hewa haitabiriki.
Kweli nilipanda bodaboda hiyo na safari ilienda mwendo kidogo huku tukipigwa na upepo mkali. Kijana huyu nilimuuliza je ni kwema? Alinijibu kuwa yeye hali yake siyo nzuri, nilimuuliza kulikoni tena? Alinijibu kuwa kwa asubuhi ya Februari 18, 2022 alipata balaa la kuwa na ugomvu na jirani yake.
Mwanakwetu, hapo kwa kuwa nilikuwa katika bodaboda hii na upepo unapiga zigizaga ili kuweza kumsikia vizuri ilibidi niyatege masikio yangu vizuri mithili ya dishi la mitambo ya simu.
Nilikaa vizuri katika siti ya nyuma ya bodaboda hii, nikiyatega masikio yangu barabara ya kuudhibiti vilivyo upepo huo ambao sikuweza kuutambua unatokea wapi kuelekea wapi.
Kijana huyu akiniambia kuwa nyumba yake inapakana na jirani mmoja ambaye ana familia kama yeye. Huyu jirani yake ni fundi wa baiskeli na afanya kazi ya kuziba pancha za pikipiki, wakati yeye ni dereva wa bodaboda, mfugaji na mkulima.f
Nilimuuliza kumbe mwezangu una ng’ombe? Alinijibu ni kweli ana ng’ombe 50 ambazo amegawiwa baada ya shangazi yake kufariki, kwani baba yake amesema kuwa yeye sasa muda ya kuchunga ng’ombe hao hana kwa hiyo katika mgao huo wa urithi wa shangazi yeye na mdogo wake walipatiwa kila mmoja ng’ombe 50 na wamepewa kila mmoja ng’ombe 15 za dharura za familia wazichunge, ndiyo kusema jumla ya ng’ombe zote ni 130, huku baba yao akiuza ng’ombe 70. Kwani shangazi yao huyo alifariki akiwa hana mtoto.
Mwanakwetu hayo nilisimuliwa huku safari ikiendelea. Kijana huyu alisema kuwa kila siku majira ya jioni kuna mke wa jirani yake ambaye ni fundi baiskeli huwa anaomba simu yake kuwasiliana na mumewe ili kumuagiza baadhi ya mahitaji ya familia yao.
Jambo hilo limekuwa likijirudia kila mara na mara nyingi kila asubuhi hutoka kwenda mgudini(kijiweni) katika kituo cha bodaboda kutafuta wateja.
“Uuze.”
Kijana huyu wa bodaboda hapo uitwa na mke wa jirani na akifika hapo anaambiwa maneno haya:
“Nalisaka nikulamse tu, ulibao?”
Akimaanisha kuwa alitaka kumsalimu tu, Je upo?
Kijana huyu wa bodaboda uaga.
“Nilibita saluni haoo.”
Akimaanisha anaenda saluni hapo.
Jambo hilo la mara ya kuombwa simu usiku kumpigia mumewe na mara asubuhi kuitana na kusalimiana kusiko na mpangilio limekuwa likimsumbua mno.
Februari 16, 2022 mke wa jirani yake alimuita na kumsalimia huku akisema jambo.
“Nene nalonga na gwegwe mdala kwago yakukomala, ama ndaule?”
Akimaanisha kuwa mbona mke wako ninapoongea na wewe huwa anakomaa sana, kwanini?
“Mbona miyago mdala gwangu asina noma?”
Kijana wa bodaboda alijibu kuwa mbona mke wang hana tabu.
Kijana huyu wa bodaboada anasema kuwa uzalendo ulimshinda kukawa na kila dalili ya yeye kuuweka kando uzee wa kanisa, kwa hiyo alimuomba mke wa fundi baiskeli na jirani yake kuwa kama kuna kuhisiana hivyo anaonaje wakimalizana?
Kauli hiyo ilipotamkwa na kijana huyu wa bodaboda ilikuwa kama bilauri ya maji baridi kwa mtu mwenye kiu kali baada ya kutembea kwenye jua kali.
Siku ya Februari 17, 2022 ilipita salama kila mmoja akienda kutafuta riziki yake, bodaboda na fundi baiskeli wote migudini. Huku mke wa fundi baiskeli akiendelea na tabia yake ileile.
Kulipokucha Februari 18, 2022 kijana huyu wa bodaboda anasema kuwa hapo ibilisi alisimama na alipokuwa anatoka kwake tu huku akikokota bodaboda hiyo na kuvuka korongo dogo ambalo limechimbika kutokana na mvua zinazonyesha.
Yule fundi baiskeli alimfuata na kumsalimia na kumuita kando na kumuuliza kwanini anamtongoza mkewe? Kijana huyu wa boda alishangaa hizo habari kufika kwa huyu jamaa, wakati mke wa huyu fundi baiskeli alikuwa ameyatengeneza mazingira hayo yeye mwenyewe kwa kumchokoa pweza katika pango lake, mbona ametoa siri?
Kijana wa bodaboda akisema kuwa huyu mke wa fundi baiskeli hana urembo wa kutongozwa nayeye na naye fundi baiskeli akisema kuwa kama mkewe mbaya kwanini amemtongoza?
Kweli walitupiana maneno mno, kijana wa bodaboda anadai kuwa aliwasha bodaboda na kuondoka zake.
Ndiyo akaelekea kijiweni na kuendelea na kazi yake ya kubeba abiria. Mimi nilikuwa abiria wa tatu kumbeba baada ya ugomvi huo, huko kwake.
“Kwa hiyo kaka mkubwa hapo nafanyaje?” Mwanakwetu niliulizwa swali na bodaboda huyo.
Kijana huyu kwanza nilimpa pole na changamoto hiyo, nikamwambia kwa kuwa suala la mke wa mtu halina utani, na kwa kuwa aliyegombana naye ni Mgogo mwenzake awajulishe wazee wa pale wanapoishi ili waitatue hiyo kesi mapema hiyo hiyo.
Maana kila mmoja na hasira yake na nilimuomba kuwa muda huo mimi niwe abiria wa mwisho kwa leo kwanza hadi akatatue shauri hilo kwa wazee wa Kigogo.
Kweli alifanya hivyo na amenijulisha kuwa wazee wa Kigogo waliitana mchana wa Februari 18, 2022 wamelizungumza na wameombana msamaha huku wazee waliotatua kesi hiyo wameomba mbuzi.
Wakati natoka kwa akina pangu pakavu saa 10 ya jioni ndiyo kijana huyu alikuwa akitoka kupeleka mbuzi ambaye walichanga yeye na fundi baiskeli kila mmoja 15,000/- na sasa amani imerudi katika makaazi yao.
Nilimwambia kuwa huyu mwanamke amuogope mno anaweza kumsababishia shida maishani mwake. Nikiwa hapo stendi mara liliwasili basi na mimi kupanda kurudi zangu Chamwino Ikulu.