………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Mkuu wa shule ya Sekondari Zogowale Tatu Mwambala ameishukuru Serikali kwa kuidhinisha Milioni 60 za kujenga vyumba vitatu vya Madarasa na ununuzi wa madawati zaidi ya 100 ambayo tayari Wanafunzi wameanza kuyatumia.
Mwambala alisema ,miundombinu hiyo imeongeza ari na moyo wa kujifunza kwani Sasa Wanafunzi wanakaa vizuri kwenye Madarasa yaliyojengwa kisasa.
Salma Shomari na Subira Amosi wanaosoma kidato cha tano walimshukuru Rais huku wakiahidi kumfurahisha kwa kusoma kwa bidii ili wapate ufaulu wa juu kama ishara ya asante kwake.
Nassoro Ally ambaye ni mzazi na aliyekuwa mjumbe wa kamati ya manunuzi alisema Madarasa hayo yamejengwa muda muafaka kwani Wazazi wengi walikuwa wakiumiza vichwa kwa michango ya matofali na viti ama madawati hasa kipindi hiki cha mwanzo wa muhula wa masomo na kwamba michango hiyo Sasa imebaki historia.
Akizungumza kwa niaba ya walimu,Mkuu wa shule Tatu Mwambala aliahidi kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu.
Halmashauri ya Mji Kibaha ilipata kiasi cha sh. milioni 940 ambazo zimejenga Madarasa 47 kwenye shule za Sekondari na kununua madawati zaidi ya 1,300.