Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya kaskazini,Chiku Issa akizungumza katika hafla hiyo.(Happy Lazaro)
Meneja ustawi afya ya wafanyakazi ujumuishaji na uwezeshaji kutoka benki ya CRDB makao makuu, Crescensia Kajiru akizungumza katika siku ya kuimarisha afya (Wellness day)kwa wafanyakazi wa benki hiyo iliyofanyika katika viwanja vya chuo cha Agha Khan kilichopo Kisongo jijini Arusha.(Happy Lazaro).
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya chuo Cha Agha Khan kilichopo Kisongo mjini hapa (Happy Lazaro)
********************
Happy Lazaro,Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha ,Said Mtanda amewataka wafanyakazi nchini kuwa na desturi ya kufanya mazoezi ili kuwa na utayari wa utendaji kazi kwa ufanisi kulingana na mazingira wanayofanyia kazi.
Aliyasema hayo jana jijini Arusha wakati akifungua siku ya kuimarisha afya (Wellness day) iliyoandaliwa na benki ya CRDB kwa ajili ya wafanyakazi wake kutoka Kanda ya kaskazini iliyofanyika katika viwanja vya chuo Cha Agha Khan kilichopo Kisongo mjini Arusha.
Mtanda alisema kuwa, swala la kufanya mazoezi ni la muhimu Sana kwa ajili ya kuimarisha afya za wafanyakazi na kuongeza ufanisi kazi huku wakiepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Mtanda alisema kuwa,endapo mazingira ya kazi yakiwa mazuri hata utendaji kazi wa wafanyakazi unaongezeka siku hadi siku kwani ni jambo la msingi .
“Unapodili na watu katika Taasisi yoyote lazima uone mahitaji yao,wanahitaji utulivu,mapumziko na kunakuwepo na mahusiano mazuri kati ya watumishi na Taasisi husika ,hivyo lazima waimarishe afya za watumishi ili wasiyumbe kwani kupata watumishi weledi na waaminifu ni changamoto katika nchi yetu,hivyo lazima tulinde afya zao ili kuongeza ufanisi zaidi.”alisema Mtanda.
Mtanda alisema kuwa,tusipowekeza kwenye Afya za watumishi wetu kinachofuata ni kuongezeka kwa umaskini ,kwani uwekezaji mzuri kuliko wote ni kujali afya za watumishi .
“kama mnataka msitembee na dozi barabarani na kujiepusha na magonjwa nyemelezi hakikisheni mnajijengea tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujiepusha na changamoto hizo zinazoweza kuepukika”alisema Mtanda.
Naye Meneja ustawi afya ya wafanyakazi ujumuishaji na uwezeshaji kutoka benki ya CRDB makao makuu,Crescensia Kajiru alisema kuwa,walishafanya programu hiyo katika kanda mbalimbali huku lengo likiwa ni kuisaidia serikali katika swala zima la kuimarisha afya za wafanyakazi pamoja na kuwepo kwa michezo na kupima afya zao bado wanawajibika kujikita katika kuimarisha afya za watumishi ambapo programu hiyo itafanyika kwenye matawi yao nchi nzima.
Alisema kuwa, wao kama wafanyakazi wa benki lazima wachukue hatua na tahadhari katika ulaji wa chakula na kufanya mazoezi ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazochangiwa na magonjwa yasiyoambukiza na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kujali afya za wafanyakazi wao.
“Tutakuwa na mwendelezo wa siku za afya katika matawi yetu kwani tunaamini afya ya akili ikiwa sawa ndio tutaweza kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yetu na kuwa na uwezo mkubwa katika utendaji kazi wetu.” alisema Kajiru.
Naye Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya kaskazini ,Chiku Issa alisema kuwa,wafanyakazi hao wanakaa kwenye viti muda mrefu na ina madhara yake hivyo mazoezi ni muhimu Sana kwa afya zao na utendaji kazi wao wa kila siku.
Chiku alisema kuwa, programu hiyo ilianza tangu mwaka jana kwa lengo la kujenga uelewa kwa wafanyakazi wake katika kuepukika na magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya mazoezi na kujua vyakula vya kutumia ili kuongeza utendaji kazi wao.