Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael akizungumza na uongozi na Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa (Hawapo pichani), Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael akiweka sahii kwenye bango la mradi wa kuboresha Kijiji cha Makumbusho kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael akisimika nguzo kuu ya nyumba ya Wazanaki kama ishara ya kuanza mradi wa Maboresho ya Kijiji cha Makumbusho
Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael akipata Maelezo ya mwonekano wa Kijiji cha Makumbusho kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Makumbusho hiyo Bw Mawazo Ramadhani Jamvi (kulia) pembeni ya Katibu Mkuu ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga
Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael kitabu cha mpango mkakati wa Taasisi hiyo
…………………………………………….
Na Mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael ameitaka Makumbusho ya Taifa kutumia fedha za miradi ya inayofadhiliwa na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 kama zilivyokusudiwa kwa maendeleo endelevu.
Dkt Francis Michael ametoa wito huo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua Mradi wa Uboreshaji wa Kijiji cha Makumbusho wa kukuza utalii wa Kiutamaduni Kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.
Pamoja na kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa kazi nzuri inazozifanya katika uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni, amesisitiza fedha za miradi hiyo zitumike kama zilivyopangwa ili kuleta matokeo chanya ya malengo ye fedha hizo.
“Nitoe maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa kuhakikisha anasimamia miradi hii kikamilifu ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa, kwa kuzingatia umuhimu wa Kijiji cha Makumbusho kwa Jamii, Wizara na Serikali kwa ujumla” alisema Dkt Michael.
Amesema Wizara itafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa na Makumbusho ya Taifa ili kuhakikisha kuwa lengo la Serikali linafikiwa.
Katibu Mkuu amesema kuwa anatambua jitihada ambazo Makumbusho ya Taifa imechukua katika kukabiliana na athari za kiuchumi zilizotokana na Uviko-19 ikiwemo kuwa na mpango wa dharura wa kurudisha shughuli katika hali yake ya awali, kwa kubuni programu na miradi ya muda mfupi na mrefu.
Hata hivyo, mchango wa Serikali umekuwa mkubwa katika kuhakikisha shughuli za Makumbusho ya Taifa, na hasa Kijiji cha Makumbusho zinarudi katika hali ya kawaida na kuziboresha ambapo kati ya TZS 2.45bn/- zilizotolewa na Serikali kwa Makumbusho ya Taifa Kijiji cha Makumbusho kimepatiwa TZS. 201,000,000.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga alieleza kuwa fedha zilitolewa kwa Kijiji cha Makumbusho zitatekeleza miradi ya Ujenzi wa Nyumba za Asili kwa kufuata Ramani ya Tanzania; Ujenzi wa maumbo ya sura ya nchi, kuakisi Ramani ya Tanzania (Bahari ya Hindi na Ziwa Victoria); Uboreshaji wa Bohari na Maabara za Mikusanyo na Uboreshaji mandhari ya nje ya Kijiji ili kuleta mvuto shawishi kwa wapita njia na kuboresha onesho la kazi za sanaa za mikono.
Dkt. Lwoga aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya utalii nchini ili iweze kuvutia wageni wa ndani nan je ya nchi.
“Tunatoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya utalii nchini.” Alisema Dkt Lwoga.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa amesema kuwa Taasisi yake itahakikisha inatekeleza miradi yote kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.