…………………………………………………………
Na WMJJWM-Dodoma,.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dkt Dorothy Gwajima amepokea Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) leo katika ofisi za Wizara hiyo mpya uliofika kwa ajili ya kujitambulisha na kuonesha utayari wa kufanya kazi na Serikali.
Akizungumza na Ujumbe huo ulioongozwa na Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF hapa nchini Bi. Shalini Bahuguna, Dkt. Gwajima amesema wizara hiyo iko tayari kufanya kazi na Shirika hilo hasa kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi katika mambo ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ya Kitanzania.
“Nimekuwa nikifanya ziara za kikazi mikoani na kukutana na Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Mtoto ngazi ya Kata na Mitaa ambapo, kilio chao kikubwa ni upungufu wa wataalamu wa maendeleo na ustawi wa jamii kwenye ngazi hiyo, hivyo sisi tunayo imani kupitia ushirikiano wenu changamoto hii itapata ufumbuzi.
Dkt. Gwajima amesema, wanatambua na kuheshimu kazi ambayo imeendelea kufanywa na Shirika hilo hapa nchini hususan katika Ulinzi wa Mtoto kabla ya kuundwa kwa Wizara hii mpya.
“Imempendeza Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, kuunda hii Wizara Maalum hivyo tunaomba ushirikiano wenu.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF nchini Bi Shalini amesema, UNICEF iko tayari kushirikiana na Serikali kufanya mapitio ya hali halisi ilivyo sasa kwenye utekelezaji wa maendeleo na ustawi wa watoto na kwa pamoja kuja na mkakati unaojibu mahitaji ya wakati wa Sasa ili kutimiza matarajio ya Mhe Rais.
Aidha, Wizara hii imeendelea kuwakaribisha na kuwapokea Wadau mbalimbali wa Maendeleo ambao wapo tayari kufanyakazi na Serikali kupitia wizara hii, huku Dkt. Gwajima akisema milango ya kushirikiana na Wadau katika kuwaleta wananchi Maendeleo ipo wazi daima.