Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) kabla ya kukabidhi leseni ya magazeti yaliyofungiwa ya Mseto, Mwanahalisi, Mawio na Tanzania Daima kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknollojia ya Habari, Nape Nnauye akikabidhi leseni ya gazeti lililofungiwa la Mawio kwa Erasto Massawe baada ya magazeti hayo kufungiwa kwa zaidi ya miaka miwili. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dar es Salaam. Anayeshuhudia kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi na kulia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile
**********************
Na Prisca Ulomi, WHMTH, DSM
Serikali imeyafungulia magazeti manne baada ya kufungiwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Hayo ameyasema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye wakati wa kikao chake na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania uliopo Dar es Salaam leo.
Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameniagiza niyafungulie magazeti yaliyofungiwa na Mhe. Rais akisema agizo lake linakuwa ni sheria, na sheria inatekelezwa.
“Leo natoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa ambayo ni Mseto, Mawio, Tanzania Daima na Mwanahalisi, hivyo ni vizuri kuondoka kwenye maneno tutende, na leseni hizo nazikabidhi leo, kifungo kimetosha, Kazi iendelee,” amesisitiza Waziri Nape
Waziri Nape amesema kuwa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye tasnia hii ni kuwa karibu nanyi, tuzungumze kwa kuwa ninyi ni wadau kwenye maendeleo ya taifa letu, semina hizi zirekodiwe, mawazo ya wanahabari yachukuliwe vizuri, ili viongozi tuyachukue na kuyafanyia kazi, tunataka tuboreshe mahusiano yaliyopo katika ya Sekta ya Habari na Serikali, ambapo ameleekeza tupitie sheria, taratibu na kanuni ili ziwe rafiki na kuwezesha utendaji kazi wa wanahabari badala ya kuwa kikwazo kwa wanahabari
Nakumbuka nikiwa Waziri nilipitia Sheria ya Habari na kuisimamia ila mazingira ya wakati ule ya mwaka 2016 na ya sasa ya mwaka 2022 ni tofauti kwa kuwa ni maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na tutakubaliana baadhi ya maeneo yaendelee na mengine tutayafanyia kazi kama vile suala la taaluma ya wanahabari tutalisogeza mbele kwa kipindi cha mwaka mmoja ili tulifanyie kazi.
Namshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kunirudisha tena nyumbani nami na wenzangu namuahidi kuwa tutatekeleza majukumu yetu ipasavyo kwa kuwa Habari na Teknolojia ya Habari ni kama damu na mwili kwa namna Sekta hizi zinavyokwenda na zinavyokua hapa duniani, namshukuru Mhe. Rais kwa kuunda Wizara hii
“Mhe. Rais amesema anawasalimu ninyi wahariri ambao ni viongozi wenzake na anawaomba muendelee kushirikiana nae kufichua uovu na kuwa jicho lake katika shughuli mbali mbali zinazoendelea nchini”, amesisitiza Waziri Nape.
Katika hatua nyingine ameiagiza Idara ya Habari – MAELEZO kushirikiana na Jukwa la Wahariri (TEF) ndani ya muda mfupi ili kuwa na kikao na wanahabari kwa malengo ya kujadiliana mapendekezo yaliyoletwa Serikalini ya kuboresha sheria zilizowasilishwa ili zipitiwe upya kifungu kwa kifungu ili kuboresha Sekta ya Habari nchini
Pia, amewashukuru wamiliki wa vyombo vya habari kwa kuwalipa waandishi wa habari waliofariki kwenye ajali ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza pamoja na waandishi waliokuwa wanaidai kampuni ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwalipa waandishi hao na Serikali itaendelea kulinda haki za waandishi wa habari ambapo Serikali itatumia sheria, taratibu, kanuni na busara katika kila jambo kwenye uendeshaji wa tasnia ya habari nchini
Aidha, Waziri Nape amezielekeza taasisi za Serikali zilizokuwa zinasita kutoa matangazo kwa vyombo vya habari, watoe matangazo, walipe madeni kwa kuwa wote tuna haki sawa, hakuna haki ya kubaguana na ikiwezekana tuweke utaratibu kwa wakubwa na wadogo ili nao wote wapewe matangazo
“Tunajenga nchi moja, nawaomba muitumie vizuri imani ya Serikali kama lipo jambo tuongeeni, juzi gazeti la Raia mwema waliandika stori kuhusu mabadaliko ya sheria ndogondogo, kutokana na mjadala uliotokea Bungeni, baadhi ya waandishi waliona mwanzo wa mchakato ila hawakuona jambo hilo limeishaje, ila mwandishi angefuatilia angetoka na stori iliyo njema, ila Spika angeenda mbali zaidi hali ingekuwa tofauti, tatizo hatuna muda wa kutafuta ukweli, nawaomba tuaminiane, kama jambo hujalielewa semeni na ni vema wahariri muwalete waandishi wenye uelewa Bungeni na wazoefu,” amefafanua Waziri Nape
Waziri Nape amesema kuwa Wizara anayoiongoza itafungua milango wakati wote, ila mwandishi ukiamua kwenda kwingine hilo la kwako mwenyewe, mkikosa habari mahali mnieleze ili tunyime fursa ya watu kupotosha habari kwa kuwa tunawalisha watu habari ambazo sio sahihi
Naye Said Kubenea wa magazeti ya Mseto na Mwanahalisi ameishukuru Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua hii kubwa ya kufungua magazeti haya ambapo magazeti yetu yalimaliza adhabu zaidi ya miaka miwili iliyopita na yalishinda kesi ila hayakuweza kurudi mtaani ila tuyaache yaliyopita sasa tugange yajayo, pia namshukuru Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi akiwa Naibu Katibu Mkuu alitusikiiza, tukachakata jambo hili na ni vizuri kwa viongozi na Serikali kusikiliza, nasi tutaenda kufanya kazi kwa kuangalia maslahi ya taifa letu kwa kuwa sisi wote ni watanzania, tutazingatia weledi, maadlii na utendaji wa kazi zetu
“Tumepata leseni, ila unaweza ukashangaa magazeti haya usiyakute mtaani kwa kuwa hali ni mbaya kwa kuwa yapo magazeti ambayo hayajafungiwa ila yamejifungia yenyewe, hivyo naiomba Serikali iangalie namna ya kuyapa ruzuku magazeti ya hapa nchini
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa kila wakati anapokutana na wahariri, anajisikia joto kwa kuwa aliwahi kuwa Mhariri na Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali ambapo vyombo vya habari kama vilivyo vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wahariri nao ni sehemu ya ulinzi na usalama kwa kupeleka habari kwa wananchi za kulinda maslahi ya taifa letu na amepokea maelekezo ya Waziri Nape ya kuifanya Sekta ya Habari kuwa bora na kuwekeza nchini na hata nje ya nchi na Wizara imeamua kuleta utulivu katika tasnia ya habari na ana amini utulivu utaifanya tasnia hii ikue hivyo amewaomba wanahabari hasa wahariri kufanya kazi na Serikali ili pale ambapo ilionekana tasnia hii ni ndogo sasa ikue na kuzifanya sekta nyingine zikue na wawekezaji wakimbilie kuwekeza nchini kwetu kwenye tasnia hii ya habari kwa kuwa tunafahamu kuwa tunapokea habari kutoka vyombo vingine vya habari duniani hivyo nasi tufanye hivyo kwa kupeleka habari bora za taifa letu kwenye mataifa mengine
Naye Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi Tanzania amemshukuru Waziri Nape kwa kuchukua jitihada hii kwa kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu sana wa kufanya kazi na Serikali na hawa ni wadau muhimu sana
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deusdedit Balile alisema kuwa ikitokea ukakutana na mfalme unamsalimia hapo hapo na ukikutana na simba unamkabili hapo hapo, hivyo naomba Serikali ipitie sheria ya vyombo vya habari ili ifanane na za wenzetu wa kimataifa na tunashukuru Waziri Nape kwa kuwa tarehe 6 mwezi Aprili, 2021 Mhe. Rais alielekeza Serikali ifungulie vyombo vya habari vilivyofungiwa vya mawio, mwanahalisi, mseto na Tanzania Daima
Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akimkaribisha Waziri Nape alimuarifu kuwa mbele yake kuna wahariri zaidi ya 70 ambao wamekutana ili kupata mafunzo ya taaluma ya habari ya kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu majukumu, taaluma na maadili ya waandishi wa habari nchini ambapo Waziri Nape aliyafungulia magazeti hayo mbele ya wahariri hao
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknollojia ya Habari