************************
Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
WANAWAKE wa Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutatua migogoro ya ardhi Ngorongoro, ili kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake na watoto ambao wamekuwa na hofu, wakiathirika na migogoro inayoendelea.
Mkurugenzi wa shirika la utetezi wa wanawake na watoto la MIMUTIE, Rose Njilo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha mashirika ya utetezi wa wanawake na watoto Ngorongoro, amesema wanawake na watoto wamekuwa wahanga wa migogoro inayoendelea.
Njilo amesema wanawake wana imani kubwa na Rais Samia Suluhu kusaidia wanawake na watoto Ngorongoro kwani wanakosa amani, watoto hawaendi shule, hakuna huduma bora za afya.
Amesema mashirika ya utetezi wa haki za wanawake na watoto, wana imani kubwa na Rais Samia Suluhu kuwa anaweza kurejesha furaha na amani kwa wanawake na watoto wa Ngorongoro na kwa kuingilia kati migogoro ya ardhi.
“Sisi tunaomba huduma muhimu zitolewe Ngorongoro kama elimu, maji, afya na chakula, amani na utulivu virejeshwe kwani kila mara migogoro imekuwa ikiibuliwa na wanaopata shida ni wananawake na watoto,” amesema Njilo.
Amesema vijana wengi wa jamii hiyo, wameondoa Ngorongoro na kwenda kufanya ulinzi katika nchi jirani za Kenya na Uganda na wengine katika miji kama Dar es Saalam, Arusha na Mwanza si kwa kupenda bali katika maeneo yao hakuna utulivu.
Mkazi wa Ngorongoro, Mariam Kibore ameitaka serikali kutatua shida za wanawake wa watoto wa Ngorongoro kwani wanaoshi maisha magumu, ikiwepo kukosa huduma muhmu.
“Tunaomba Serikali itusaidie sisi wanawake, tuondokane na hofu kila siku hatujuwi kesho itakuwaje, watoto hawasomi shule kwa amani,” amesema.
Wilaya ya Ngorongoro imekuwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu Tarafa ya Loliondo na ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.