Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa kikao na ujumbe wa Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kuhusu fedha za mkopo kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II), jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dk. Jilly Maleko na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Bw. Tusang Sylvain Tusanga baada ya kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika Bw. Tusang Sylvain Tusanga, akizungumza wakati wa kikao na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu fedha za mkopo kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II), jijini Dodoma. Kulia ni Mhandisi Onesphory Kamukuru kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dk. Jilly Maleko na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. James Msina, wakifuatilia kikao kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, (wa tano kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dk. Jilly Maleko, (wa tano kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika Bw. Tusang Sylvain Tusanga, (wa nne kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Burundi uliojadili kuhusu utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II), jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, akibadilishana mawasiliano na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Bw. Tusang Sylvain Tusanga, baada ya kikao kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II), jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa kikao na ujumbe wa Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II), jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Bw. Tusang Sylvain Tusanga, akifuatiwa na Mhandisi Namkuru Onespheni kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM- Dodoma)
*********************
Na. Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
TANZANIA imeahidi kuunga mkono utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingiraya Bonde la Ziwa Tanganyika kutokana na umuhimu wa program hiyo kwa wananchi wa nchi nne zinazonufaika na program hiyo ikiwemo Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Rwanda na Zambia.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) uliofika ofisini kwake kuomba idhini ya Serikali ya kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Alisema kuwa Serikali inaunga mkono kuanza kwa Awamu ya Pili ya Programu ya Kikanda ya Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II) baada ya Awamu ya kwanza ya program hiyo iliyokamilika mwaka 2014 kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wanaozunguka Bonde la Ziwa Tanganyika katika nchi hizo nne za Kikanda.
“Katika kuandaa mradi wa awamu ya pili tumekubaliana kuwa sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango tutaratibu Wizara nyingine ili tupate vipaumbele ambavyo tutaviwasilisha katika Taasisi yake ili iweze kuviunganisha na vile vya nchi wanachama kisha kuiwasilisha katika Benki ya Maendeleo ya Afrika ili waweze kufanya upembuzi yakinifu ili miradi hiyo ikitekelezwa iweze kuwiana na malengo ya kupunguza umasikini kwenye jamii inayozunguka eneo hilo” alisema Bw. Tutuba.
Alisema kuwa katika Awamu ya kwanza, Mamlaka ya Hifadhi ya Ziwa Tanganyika ilitekeleza mradi wa ujenzi wa masoko eneo la Kibirizi Mkoani Kigoma ambapo wameweka vifaa mbalimbali vya uhifadhi wa Samaki na Dagaa, maeneo ya kukaushia Samaki na maghala ya kuhifadhia samaki.
Bw. Tutuba alisemakuwa miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule 22, Vyoo kwenye shule 18, miradi mitano ya vituo vya afya, nyumba za watumishi kwenye vijiji viwili na Zahanati moja na miradi 10 ya maji katika vijiji vinavyozunguka Ziwa Tanganyika.
Miradi mingine ni ujenzi wa kilomita 65.6 za barabara, madaraja mawili na kufanya kampeni 180 za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ukiwemo Ukimwi.
Aidha, Bw. Tutuba alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa programu hiyo, Tanzania imekuwa ikichangia kila mwaka dola 303,900 ambapo kiwango hicho kinachangiwa na kila nchi mwanachama na kwamba miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kupunguza umasikini kwa wananchi.
Bw. Tutuba alisema kuwa Tanzania iko tayari kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Programu hiyo kutokana na fedha zitakazopatikana kwa njia ya mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwa miradi iliyotekelezwa kupitia ushirikiano huo imeleta maendeleo uendelevu ya Mazingira katika Ziwa Tanganyika na inagusa sekta mbalimbali za kuondoa umasikini kwa wananchi.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Burundi, ambaye anasimamia maslahi ya Tanzania katika Sekretarieti ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika yenye Makao yake Makuu nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jilly Maleko, alisema kuwa Lengo la ziara ya Sekretarieti hiyo nchini ni kufanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa kupata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Kikanda ya Uhifadhi wa Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika (PRODAP II).
Alisema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ambayo ilimalizika mwaka 2014, kwa upande wa Tanzania ulitekelezwa chini ya uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa gharama za dola za Marekani milioni 7.2 kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Alisema kuwa Mamlaka ya LTA imefanya mazungumzo na AfDB kuhusu uwezekano wa kutekelezwa kwa PRODAP II kwa msaada au Mkopo wa masharti nafuu na tayari Sekretarieti hiyo imefanya mazungumzo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia ambazo zimeonesha nia ya kuendelea na utekelezaji wa programu hiyo kwa awamu ya pili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Bw. Tusang Sylvain Tusanga, alizishukuru nchi wanachama hususani Tanzania kwa kuonesha nia thabiti ya utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa michango yake ya kila mwaka kikamilifu tangu mwaka 2000.
Alisema ushirikiano huo umeleta tija katika Bonde la Ziwa Tanganyika na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi miundombinu ya barabara, afya, elimu, uvuvi na hifadhi ya mazingira.