Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akimkaribisha Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina Ikulu Chamwino mkoani Dodoma Kwaajili ya mazungumzo baina yao. Februari 8,2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Februari 8,2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina pamoja na ujumbe wake mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yao Ikulu Chamwino mkoani Dodoma. Februari 8,2022.
***************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 8 Februari 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais amemshukuru Rais wa AfDB kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa nchi ya Tanzania kwa kutoa ufadhili wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ya Ujenzi wa miundombinu na usafirishaji,miradi ya kilimo pamoja na Nishati. Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushirikiano ambayo yamepelekea kuimarika kwa sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.
Makamu wa Rais amempongeza Dkt. Adesina kwa kuchaguliwa kwake tena kuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina ameipongeza serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza taifa vema pamoja na kuwa Rais wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania pamoja na kuwa Rais na kiongozi mkuu wa serikali mwanamke aliopo kwa sasa Barani Afrika. Dkt Adesina amesema Rais Samia amekua mfano na alama aliefufufua ndoto za wanawake nchini na barani Afrika hivyo Benki ya Maendeleo ya Afrika itaendelea kumuunga mkono katika kuwaleta maendeleo watanzania.
Dkt. Adesina ameipongeza serikali kwa maendeleo makubwa iliofikia licha ya athari za Uviko 19 pamoja na kuendeleza miradi ilioanzishwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika ikiwemo ujenzi wa Barabara ya mzunguko ya kilometa 112 pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato mkoani Dodoma.
Amesema wakati wote Tanzania imekua mshirika mzuri wa Benki hiyo na kutumia vema fedha za miradi zinazoletwa nchini katika kuendeleza sekta mbalimbali. Dkt. Adesina amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika itatoa mchango wake kwa Tanzania katika kuinua wanawake, vijana sekta ya kilimo na miundombinu.
Aidha amesema katika kukabiliana na changamoto za afya barani Afrika ikiwemo Uviko 19, Benki ya Maendeleo ya Afrika inatarajia kufadhili miradi ya ujenzi wa viwanda vya dawa pamoja na kuunga mkono upatikanaji wa chanjo zinazozalishwa barani afrika.