…………………………………………………
Na Angela Msimbira BUNDA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa kuwezesha ujenzi wa madarasa 15,000 ili wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza waweze kusoma bila msongamano.
Akiongea leo wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kutibu maji Waziri Bashungwa amesema kwa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu serikali imeweza kujenga shule shikizi 3000 ili watoto hao waweze kupata elimu karibu na maeneo yao.
Amefafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 240 zimetumika katika ujenzi wa madarasa 12,000, shilingi bilioni 60 zimetumika katika ujenzi wa shule shikizi 3000 na shilingi bilioni 80 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya watoto wenye mahitaji maalum nchini.
Waziri Bashungwa amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum za Sayansi kwa wasichana kwenye mikoa 10 ambapo mikoa 16 iliyobaki fedha zitatengwa kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 lengo likiwa ni kuboresha sekta ya Elimu nchini.
Kuhusu elimu bila Malipo Waziri Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kiasi cha shilingi bilioni 312 zilitengwa kwa ajili ya elimu bila malipo ambapo mpaka sasa ikiwa ni nusu mwaka kiasi cha shilingi 140.43 kimepelekwa kwenye Mikoa yote nchini
Aidha, Waziri Bashungwa amesema katika kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo,tayari amewasiliana na Ofisi ya Makaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ili kutatua changamoto hiyo.