Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akizungumza katika Kongamano la wadau katika kupambana na vitendo vya ukeketaji lililofanyika Wilayani Tarime Mkoani Mara. Baadhi ya wadau wakifuatilia mada mbalimbali katika Kongamano la wadau katika kupambana na vitenpo vya ukeketaji lililofanyika Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akijadiliana jambo na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Grace Mwangwa wakati wa Kongamano la wadau katika kupambana na vitendpo vya ukeketaji lililofanyika Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Baadhi ya Wanafunzi kutoka Shule mbali mbali katika Halmashauri ya Tarime wakiwa wanasikiliza kwa makini Hotuba ya Naibu Katibu Mkuu Amon Mpanju wakati wa Kongamano la kupinga Ukatili.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
*******************************
Na WMJJWM- Tarime Mara
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju amewatahadharisha baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi wilayani Tarime Mkoani Mara, ambao sio waaminifu wanaotoa taarifa za Serikali katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji kwamba Serikali haitawavumilia na badala yake Sheria itachukua Mkondo wake wakibainika.
Ameyasema hayo wilayani Tarime, mkoani wa Mara, alipokuwa akifungua kongamano la wadau wanaopinga vitendo vya Ukatili wa ukeketaji nchini ikiwa ni muendelezo wa jititahada za Serikali katika mapambano dhidi ya ukeketaji.
“Tunazo taarifa za baadhi ya askari wetu wa Jeshi la Polisi kanda Maalum Tarime- Rorya kuhusika na kutoa taarifa kwa wanaofanya vitendo vya ukeketaji Wilayani hapa na kukwamisha jitihada za Serikali na wadau katika kukomesha vitendo vya ukeketaji nchini” alisema Mpanju.
Aidha ameitaka jamii na wadau kuendelea kuunganisha nguvu katika kuwalinda Watoto wa kike na wanawake dhidi ya vitendo vya Ukeketaji na kusisitiza kuwa makundi yote katika jamii yana wajibu wa kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi ya vitendo vya Ukeketaji.
“Mimi niseme haiwezekani ukawa mtumishi wa Serikali alafu ukahujumu jitihada za Serikali katika kupambana na vitedo hivi vya ukeketaji vinavyoharibu na kupoteza ndoto za watoto wetu wa kike, vitendo vya ukeketaji vinafanyika, watu wanapita mbele ya vituo vya Polisi na Polisi wapo, nasema kwa sasa suala hili haliweze kuvumilika tena” alisema Mpanju
Pia amewataka Viongozi wa Kimila kuachana na Mila zilizopita kwa wakati ili kuwaokoa Watoto wa kike na vitendo vya Ukeketaji ambavyo vinasababisha Watoto wengi kupoteza ndoto zao katika maisha.
Awali akitoa salam za Mkoa wa Mara kuhusiana na siku ya Kupinga Ukeketaji, Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa huo Neema Ibamba, amesema Mkoa umeendelea na jitihada za mapambano dhidi ya na wamefanikiwa kwa asilimia 30, ambayo ilitokana na jitihada za pamoja baina ya Serikali na wadau.