Katibu wa kikundi cha Faraja cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lidya Mollel akisoma taarifa ya kikundi hicho wakati walipokabidhi chumba kimoja cha darasa moja la shule ya msingi Mirerani walilokarabati kwa gharama ya shilingi milioni 1.6.
……………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
KIKUNDI cha Faraja cha Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kimekarabati darasa moja la shule ya msingi Mirerani kwa gharama ya shilingi milioni 1.6.
Katibu wa Faraja, Lidya Mollel akisoma taarifa wakati wa kukabidhi darasa hilo kwa Diwani wa kata ya Endiamtu Lucas Zacharia amesema waliamua kulikarabati kama hisani kwa jamii.
Mollel amesema ili kuunga mkono jitihada za dhati za Rais Samia Suluhu Hassan ya ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali hapa nchini nao wakaiga jambo hilo la maendeleo.
Amesema kikundi hicho huwa wanakutana mara moja kwa mwezi kwenye shule hiyo ndiyo sababu wakakarabati daraja moja la shule hiyo ya msingi Mirerani.
Amesema ukarabati uliofanyika ni kuweka sakafu, kupiga plasta ndani sehemu zote zilizobomoka, kupiga puchi ya nje na ndani, ukuta wa ndani wa darasa hilo na kupiga rangi ndani.
“Tunamshukuru mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mirerani Tunisia kwa ushirikiano aliotupatia na kukubali ombi letu la kuruhusu kufanyia vikao hapa shuleni,” amesema Mollel.
Diwani wa kata ya Endiamtu Lucas Chimba Zacharia amewapongeza wanachama wa kikundi cha Faraja kwa kufanikisha ukarabati wa darasa moja la shule ya msingi Mirerani kwa gharama zao.
“Ninawashukuru na kuwapongeza wanachama wa Faraja kwa kuamua kuiunga mkono Serikali na kukarabati darasa moja ambalo lilikuwa linawapa wakati mgumu wanafunzi kusoma,” amesema Luka.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mirerani Tenisia Katukuru aliwapongeza wanachama wa Faraja kwa kukarabati darasa hilo moja la shule yake kwani hivi sasa wanafunzi wanasoma vizuri.
“Awali darasa hilo lilikuwa limechakaa hata kuvuta dawati ilikuwa shida kwani kulikuwa na mabonde mabonde hivyo wanafunzi kutokuwa na wasaa mzuri wa kusoma,” amesema.