………………………………………………..
Na WMJJWM- DODOMA
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, amepokea Ujumbe wa Baraza la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCongo), ikiwa ni Ziara yao ya kwanza tangu kuundwa kwa Wizara hiyo mapema Mwezi Januari, 2022.
Uongozi huo wa NaCONGO ulioambatana na Wajumbe 25 kati wajumbe 30 wanaounda baraza hilo, wameeleza dhamira yao katika kufanya kazi na Serikali kupitia Wizara hiyo ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula, akizungumza wakati wa Ziara hiyo, amewapa Wajumbe hao mwelekeo wa Wizara hiyo mpya inayowaratibu na kupokea taarifa yao ya utendaji pamoja na kupata maoni yao kuhusu sheria taratibu na miongozo ya uratibu wa NGos.
Kupitia kikao hicho Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula, amesimamia na kuwezesha zoezi la makabidhiano ya ofisi ya Nacongo toka kwa viongozi waliomaliza muda wao kwenda kwa viongozi wapya.
Makabidhiano hayo pia yamehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi maalum ili kushuhudia mwenendo mzima wakubadilishana Madaraka kutoka Uongozi uliomaliza muda wake kwenda kwa Viongozi wapya.
“Niwatakie utekelezaji mzuri wa majukumu yenu mnapochukua jukumu la kuiongoza Nacongo, ni imani yangu, pale Uongozi uliopita ulipishia mtaendeleza mazuri kwa manufaa ya taasisi ya Nacongo lakini pia manufaa kwa Taifa” alisema Dkt. Chaula.
Kwa upande wake rais wa Baraza la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCongo) Dkt. Lilian Badi amemuhakikishia Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula kuwa watashirikiana na Wizara katika kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yabaratibiwa vizuri ili kuongeza nguvu katika juhudi za Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii kwa kuhakikisha miradi wanayotekeleza inainufaisha jamii.