************************
NM-AIST, Arusha
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Emmanuel Luoga ameeleza kuwa matokeo yatakayopatikana kutokana na utafiti wa Jaribio la kuzuia Sumu Kuvu (Mycotoxins Mitigation Trial Project) yatasaidia kuonesha uhusiano kati ya sumu kuvu na udumavu kwa watoto wachanga.
Prof. Luoga amesema hayo leo Februari 3, 2022, jijini Arusha wakati akifungua kikao cha Wataalamu wa Mradi wa Jaribio la Kuzuia Sumu Kuvu unaoshirikisha watafiti kutokea Taasisi ya Nelson Mandela na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dodoma.
“Lengo kuu la mradi huu ni kuthibitisha kwa kutumia tafiti na majaribio ya kimaabara, dhana ya kwamba ulaji wa vyakula vyenye sumu kuvu iliyozidi kiwango kinachovumilika kwa muda mrefu unachangia udumavu kwa watoto wachanga” amesema Prof. Luoga
Ameendelea kufafanua kuwa, suala la udumavu ni janga la Taifa kama ilivyoanishwa kwenye “Tanzania National Nutrition Survey (TNNS, 2018) ambapo inaeleza asilimia 31.8 ya watoto wa Tanzania ni wadumavu hivyo kusababisha ukuaji hafifu wa akili na utambuzi.
“Utafiti huu ni wa manufaa sana kwetu wanasayansi, wana-Kongwa na Taifa kwa ujumla kwa kuwa utatoa takwimu muhimu kwa Taifa na wadau wa maendeleo katika kupambana na suala zima la lishe na afya” amesisitiza Prof. Luoga
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amesema kuwa matokeo na mapendekezo yatakayotokana na utafiti huo yatasaidia katika kuishauri Serikali namna ya kutatua tatizo la sumu kuvu nchini.
Naye Mratibu wa Mradi kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Dr. Neema Kassim ameeleza kuwa, matokeo ya awali ya utafiti yaliyofanywa kwa watoto wachanga wenye umri wa miezi 6 yanaonyesha udumavu kwa asilimia 20.
Aidha Dkt. Neema ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2017 kwa vituo vya afya na zahanati zote 52 za Wilaya ya Kongwa. Utekelezaji wa awamu ya kwanza ulianza Juni, 2017 hadi Juni 2018 na awamu ya pili umeanza Julai 2018 hadi Juni 2022 lengo ikiwa ni kuangalia ubora wa chakula ikijumuisha sumu kuvu na ukuaji wa mtoto mchanga.
Mradi wa Jaribio la Kuzuia Sumu Kuvu (Mycotoxins Mitigation Trial Project) unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha, Chuo Kikuu Cha Cornell Cha nchini Marekani pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Jijini Dodoma.