NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
UKUTA wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa unadaiwa kuvunjwa na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Mpito ya msikiti huo iliyoundwa na RITA wakishirikiana na machinga ili wajengewe vibanda vya biashara.
Uzio huo unadaiwa kuvunjwa Januari 28,mwaka huu, majira ya kati ya saa 4:00 na 5:00 usiku wa kuamkia Januari 29 na baadhi ya kundi la watu na kusababisha taharuki kwa waumini wa msikiti huo.
Katika tukio hilo watu wawili walikamatwa na polisi wakidaiwa kuvunja uzio wa Msikiti huo Mkuu wa Ijumaa, mmojawapo ni kiongozi wa kamati ya mpito ya msikiti huo iliyoundwa na Wakala wa Usajili,Udhamini na Ufilisi (RITA), Abdul Majid Kigimbo na fundi Muashi mmoja jina linahifadhiwa.
Watuhumiwa hao walikamatwa na kufikishwa kituo Kikuu cha Polisi Kati Wilaya ya Nyamagana,Januari 28, mwaka huu, majira ya saa 5:00 usiku na kufunguliwa kesi ya kuharibu mali iliyopewa jalada namba MZ/RB/583/2022.
Akizungumzia tukio hilo jana kwa niaba ya waumini wa Msikiti wa Ijumaa,Sheikhe Abdallah Amin Abdallah,alisema kuvunja uzio wa msikiti kunawahusisha baadhi ya viongozi wa kamati ya mpito iliyoundwa na (RITA) wakishirikiana na machinga (wafanyabiashara wadogo) kwa ahadi ya kujenga vibanda vya (maduka) biashara.
“Kinachogomba hapa ni maslahi ya kundi la wachache,wamevunja uzio ili wajenge vibanda vya maduka kwa ajili ya machinga wapate fursa ya kufanya biashara baada ya kuondolewa na Halmashauri ya Jiji,” alisema Sheikhe Abdallah.
Alisema waislamu na waumini hawako tayari kuona msikiti huo uliojengwa kwa nguvu (fedha) za marehemu babu yake kisha kuutoa Wakfu kwa ajili ya Ibada,unajengwa maduka ya biashara huko ni kuharibu fadhili za mzee huyo.
Sheikhe Abdallah alisema mpango huo ovu unaoongozwa na kuchochewa na baadhi ya viongozi wa kamati ya amani ya viongozi wa dini,unalenga kuvuruga amani na kuiomba serikali kuingilia kati na kuwachukulia hatua wote waliojificha nyuma ya kadhia hiyo na wakimatwa nia yao itafahamika.
Alisema kama kuna mkono wa mtu kwenye mgogoro huo wako tayari kuufikishakwa Rais Samia Suluhu Hassan,haiwezekani nyumba ya Ibada yakajengwa maduka tena bila kibali cha Halmashauri ya Jiji hivyo hawatakubali kuona wakfu ukivunjwa kwa maslahi ya kundi la wachache kujenga maduka eneo la ibada.
Akiwa kwenye mkutano wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini,Imamu wa Msikiti huo,Sheikhe Hamza Mansour,alisema makundi yanayoleta migogoro kwenye taasisi watafutwe wahusika.
“Tuna marekebisho ya ukuta wa msikiti wetu,ukuta ukisimama tutafute kibali,lakini usiku wamefika watu wakazuia.Mfano yupo ndugu yetu Mashaka Baltazar,mwandishi wa habari mkongwe (akanitaja),tuandike habari za uhalisia,watafute wahusika,”alisema Sheikhe Hamza.
Hata hivyo, baada ya mkutano huo alipotafutwa kwa mara kadhaa kwa simu kuzungumzia tukio la kuvunjwa kwa uzio wa msikiti, Imamu Hamza hakuwa tayari kupokea kwa siku mbili hata alipotumiwa ujumbe mfupi kupitia simu yake hakupokea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Ramadhan Ng’anzi alipoulizwa kushikiliwa kwa watu hao wawili,wakidaiwa kuvunja uzio wa Msikiti wa Ijumaa, alisema ameiachia kamati ya usuluhishi ya Mufti inayoshughulikia mgororo huo na kwamba pande mbili zinazohusika zimeitwa.
“Tumeona hilo halina maslahi kwa jamii kwa sababu kuna mgogoro wa pande mbili, mgogoro unaoshughulikiwa na kamati ya Mufti,hivyo tumeona kwanza tuiachie kamati ifanye kazi yake tusije kui pre-empt,” alisema.
Msikiti Mkuu wa Ijumaa ulijengwa mwaka 1903 na Sheikhe Amin Abdallah kwa fedha zake,aliutoa wakfu kabla ya kufariki mwaka 1938 ambapo uliongozwa na mwanaye Sheikhe Abdallah Amin kisha mwaka 1957 iliundwa bodi ya wadhamini ya msikiti huo.