Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud aliyevaa (Shati jeupe) na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheri wakiwa katika Ziara ya kutembelea eneo la Kihinani huko Wialaya ya Magharibi “A”.
****************
Na Mwashungi Tahir Maelezo 25-8-2019.
Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina dhamira nzuri kwa wananchi wake katika kujiendeleza maisha yao.
Ameyazungumza hayo wakati wa ziara ya Wilaya ya Magharib “A” alipokuwa akitembelea eneo la Kihinani la Ushirika wa maisha gemu akiangaliya shughuli za waaanika dagaa na kuwapongeza kwa kuendelea na shughuli zao.
Amesema Serikali haikusudii kumkandamiza mwananchi ila ina lengo la kumuwekea mwananchi mazingira mazuri katika kuendelea na harakati zake za kujitafutia rizki zake za kihalali .
“Serikali yetu ni Serikali inayowapenda wananchi wake wawe na amani katika ufanyaji wao wa kazi kwa kujiajiri wenyewe na kujipatia riziki zao za kihalali na kuendeleza maisha yenu”alisema Waziri Kheir.
Aidha amewapongeza kwa kufuata ushauri wa Serikali ya kuwaondosha katika eneo la Malindi na kuwaleta eneo la Kihinani kwa nia ya kuendeleza shughuli za biashara zao kwa ufanisi zaidi.
Pia aliwataka wawe wastahamilivu baada ya kutoa changamoto zao ambazo zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi sehemu hiyo na kuwaahidi kuzitatua kwa awamu.
Kwa upande wake Katibu wa Ushirika wa maisha gemu kihinani Nasib Abdullah Khamis alisema changamoto zinazowakabili ni pamoja na ukosefu wa miundo mbinu ikiwemo barabara na kutengenezewa daraja la kudumu.
Akitembelea Kituo cha Mbuzini aliwataka viongozi wa Wilaya ya Magharibi “A” kukaa kwa pamoja na kutafutia ufumbuzi kituo hicho ili kiweze kumalizika kabla ya uchaguzi 2020 ikiwa ni Agizo la Rais la kutaka Hospitali hiyo iwe ya Wilaya.
Hata hivyo aliuomba uongozi wa Wilaya hiyo kutowaruhusu wananchi kuvamia katika sehemu hiyo kwani eneo hilo linatarajiwa kuwa hospitali ya Wilaya.
Vile vile ziara hiyo katika Mkoa wa mjini Magharibi, Wilaya ya Magharib “A” iliendelea kwa kutembelea sehemu mbali mbali ikiwemo Skuli ya Sharifu Msa, kituo cha Afya Chuini, na cha Afya Mbuzini.