…………………………………………….
- 1. UTANGULIZI Katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma za Mawasiliano nchini, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya maboresho madogo ya Kanuni za Miundombinu ya Utangazaji kidijiti na Kanuni za Leseni za mwaka 2018. Maboresho ya Kanuni hizi yana lengo la kuboresha mazingira ya utoaji huduma nchini, kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za Mawasiliano ya kielektroniki na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
- 2. MABORESHO YALIYOFANYIKA
2.1. Kwa Huduma za Utangazaji (Redio na Televisheni)
2.1.1 Mabadiliko yamefanyika kwenye Kanuni Na. 16 ya Kanuni za Miundombinu ya
Utangazaji kidijiti, 2018 ili kuruhusu chaneli za televisheni za kulipia ziweze kurusha matangazo ya kibiashara (yasiyozidi dakika 5 kwa saa). Kabla ya maboresho haya ya Kanuni, chaneli za televisheni za kulipia hazikuruhusiwa kuweka matangazo kibiashara.
Lengo la kuruhusu matangazo ya kibiashara kwenye chaneli za televisheni za kulipia:
(a) Kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji yanayoendana na uhalisia wa
biashara ya maudhui ya ndani ya kulipia; na (b) Kuhamasisha na kuchochea utengenezaji wa maudhui ya ndani.
2.1.2 Mabadiliko yamefanyika kwenye Kanuni Na. 18 ya Kanuni za Miundombinu ya
Utangazaji kidijiti, 2018 ili kuruhusu chaneli za televisheni za kutazamwa bila kulipia (Free to Air) zioneshwe bila kulipia kwenye visimbuzi vyote nchini.
Kabla ya maboresho haya ya Kanuni, chaneli za kutazamwa bila kulipia hazikuruhusiwa kuoneshwa kwenye visimbuzi vya kulipia nchini.
Lengo ni:
(a) Kuongeza wigo wa ufikiwaji wa habari kwa wananchi ambapo visimbuzi
vya chaneli za kulipia vitaweza kuonesha chaneli zisizo za kulipia bila malipo; na
(b) Kuondoa uhitaji wa kuwa na visimbuzi vingi.
2.1.3 Mabadiliko yamefanyika kwenye Kanuni Na.29 ya Kanuni za Miundombinu ya
Utangazaji kidijiti, 2018 ili kuruhusu chaneli za televisheni za kulipia kurusha matukio mubashara (live events). Kabla ya marekebisho haya matukio mubashara yaliruhusiwa kwa televisheni za kutazamwa bila kulipia pekee;
2.1.4 Mabadiliko yamefanyika kwenye Jedwali Na.1 la Kanuni za Leseni, 2018 ili
kufuta ada ya masafa kwa wenye miundombinu ya utangazaji kidijiti (Multiplex Operator) ili kuleta nafuu kwa wawekezaji kwenye eneo hili;
2.1.5 Mabadiliko yamefanyika kwenye Jedwali Na.1 la Kanuni za Leseni, 2018 ili
kuanisha aina mpya ya leseni maalum kwa watoa huduma wanaokusanya maudhui (Content Aggregators). Lengo la mabadiliko haya ni kurahisisha utoaji wa leseni na pia kuchochea na kuhamasisha utengenezaji na ukusanyaji wa maudhui ya ndani na hivyo kuongeza ajira. Kabla ya mabadiliko haya kulikuwa na leseni za utoaji maudhui na miundombinu ya maudhui pekee;
2.1.6
Mabadiliko yamefanyika kwenye Kanuni Na.8 na Jedwali Na.1 la Kanuni za Leseni, 2018 ili kubadili leseni ya vituo vya utangazaji vya kijamii kuwa leseni ndogo. Hii ina lengo la kuchochea uanzishaji wa vituo vya utangazaji vya kijamii katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za utangazaji hasa wa redio;
2.1.7
Mabadiliko yamefanyika kwenye Kanuni Na.3 na Jedwali Na.1 la Kanuni za Leseni, 2018 ili kuruhusu utangazaji wa maudhui ya elimu kwa mujibu wa mitaala iliyoidhinishwa. Mabadiliko haya yamelenga kuruhusu uanzishaji wa chaneli za televisheni au vituo vya redio maalum kwa ajili ya vipindi vya elimu, pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye elimu. Mabadiliko haya yamelenga kusogeza na kurahisisha utoaji wa huduma za elimu nchini.
2.2. Kwa Huduma za Mawasiliano ya Simu na Intaneti
(a) Mabadiliko yamefanyika kwenye Sehemu ya Kwanza ya Jedwali Na.1 la
Kanuni za Leseni, 2018 ili kuboresha mfumo wa leseni katika eneo la vituo vya kuhifadhia taarifa nchini (Public Data Centre). Lengo ni kuongeza wigo
wa uwekezaji katika huduma za mawasiliano hasa katika masuala ya kuhifadhi taarifa kutokana na ongezeko la huduma mtandao (kama vile cloud computing services);
(b) Mabadiliko yamefanyika kwenye Sehemu ya Kwanza ya Jedwali Na.1 la
Kanuni za Leseni, 2018 ili kuainisha aina mpya ya leseni kwa ajili ya vituo vya maingiliano ya Intaneti(Internet exchange Points). Maboresho haya yatawezesha kuainisha vigezo vya kiufundi vya miundombinu ya vituo vya maingiliano ya Intaneti ili kurahisisha mawasiliano;
(C) Mabadiliko yamefanyika katika Sehemu ya Nne ya Jedwali Na.1 la Kanuni
za Leseni, 2018 ili kuboresha usimamizi katika eneo hili na kuwatambua mafundi simu;
(d) Mabadiliko yamefanyika kwenye Sehemu ya Tatu ya Jedwali Na.1 la
Kanuni za Leseni, 2018 ili kuongeza aina mpya ya leseni ndogo kwa ajili ya huduma mtandao (e–services). Lengo la mabadiliko haya ni kutambua huduma mpya za mtandao na kuweka mazingira wezeshi kiusimamizi; na
(e) Mabadiliko yamefanyika kwenye Jedwali Na.1 la Kanuni za Leseni, 2018 ili
kupunguza baadhi ya ada za leseni. Lengo la mabadiliko haya ni kupunguza gharama za uwekezaji na uendeshaji kwa watoa huduma.
2.3. Leseni za Posta na Usafirishaji wa Vipeto (Postal and Courier Services)
Mabadiliko yamefanyika kwenye Jedwali Na.1 la Kanuni za Leseni, 2018 ili kupunguza baadhi ya ada za leseni za posta na usafirishaji wa vipeto. Lengo la mabadiliko haya ni kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma na kuvutia uwekezaji zaidi kwenye eneo hili.
HITIMISHO Maboresho ya Kanuni ni suala muhimu katika kuhakikisha utoaji wa huduma za mawasiliano unaendana na mabadiliko ya teknolojia na uhalisia wa mazingira yaliyopo.
Pamoja na maboresho haya, ni dhamira ya Serikali kuendelea kufanya maboresho ya Kanuni kila itakapohitajika.