………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Halmashauri ya Mji Kibaha inaendelea na zoezi la uhamasishaji wa wazee wenye miaka 60 na kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo yanayoanishwa kwa ajili ya kupigwa picha zitakazowekwa kwenye vitambulisho vyao vya matibabu bure wanapopatwa maradhi kiafya.
Zoezi limeanza wiki lililopita kwenye kata ya Mkuza ambapo tayari wazee takribani 500 wameshapigwa picha zao.
Zoezi hili linatarajiwa kutekelezwa kwenye Mitaa 73 na kata zote 14 zinazounda Halmashauri ya Mji Kibaha na ,tarehe 31 Januari litafanyika kwenye kata ya Mbwawa.
Kidawa Kindamba alipongeza kufanyika utambuzi wa wazee na kupatiwa vitambulisho akisema kuwa binadamu anapofikisha umri mkubwa anakuwa rafiki wa maradhi na kwamba zoezi hili limethibitisha kuwa Serikali ya Mama Samia inatambua umuhimu wa wazee na Mchango wao serikalini.
Mkurugenzi wa Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alisema kuwa, Halmashauri ya Mji inawathamini wazee na kwamba utawekwa utaratibu maalum wa wazee kwenye sehemu zote za matibabu ili wazee wanapofika watazamwe kwa wepesi na kwamba zoezi hilo litakuwa endelevu.