*************************
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Dawati la jinsia la jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeshauriwa kuendelea kutoa elimu sahihi katika jamii juu ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili wa kijinsia.
Hayo yamezungumzwa kwenye kikao cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga na wadau kutoka katika taasisi mbalimbali ambacho kililenga kufanya tathmini ya vitendo vya ukatili kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania ‘WFT’ ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto..
Akizungumza katika kikao hicho mkuu wa kituo cha Polisi Mkoa wa Shinyanga SP. Grace Salia amewataka wazazi kuendelea kuwasimamia watoto na kuwapatia haki zao za msingi ili kukua katika maadili mazuri.
SP. Salia amesema mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18 ambapo amesema sheria ya elimu inamtaka mzazi au mlezi kuhakikisha mtoto mwenye umri wa miaka saba (7) anaanza kusoma shule ya msingi huku akisema ni wajibu wa mzazi au mlezi kuhakikisha mtoto anahudhuria shule kila siku.
Salia amesema mzazi au mlezi anayeishi na mtoto akishidwa kumuhudhurisha shule na kusimamia malezi ya yake sheria inasema mtu huyo anafungwa miaka mitano au anatoa faini ya Milioni kumi (10) au vyote kwa pamoja.
Katika kikao hicho wakili wa serikali Mkoa wa Shinyanga Immaculata Mapunda ametaja sheria na mazingira ya mtoto kufanyakazi ambapo amesema mtoto anaruhusiwa kufanyakazi masaa yasiyozidi sita (6).
“Sheria ya mtoto inakataza mtoto kufanyakazi sosote ambazo zitamlazimisha mtoto kuingia katika shifti za usiku lakini pia katika mazingira ambayo ni hatarishi mfano kazi za uvuvi, kwenda kwenye bahari, kazi za kwenye madini, kubeba vitu vizito pamoja na kufanyakazi katika mazingira ya kemikali”.
“Basi sisi kama wadau inapoonekana katika mazingira hayo hayajaendana kutokana na matakwa ya kisheria tunaruhusiwa kuwafungulia hao watu mashitaka na kuripoti katika sehemu husika”.
Mratibu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Shinyanga, Mkaguzi wa Polisi Analyse Desdery Kaika ameeleza mafanikio ya mashauri Mahakamani kwa kipindi cha Mwaka mmoja 2021 katika Wilaya ya Shinyanga ambapo amesema ni mashauri 19 ambayo yalipata mafanikio Mahakamani huku 9 ni kesi za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kaika amesema katika mashauri 9 ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yalipata mafanikio Mahakamani yakihusisha kesi mbalimbali ikiwemo kubaka na kumpa mimba Mwanafunzi.
Baadhi ya wadau walioudhuria katika kikao hicho wamepewa nafasi kwenye vikundi kujadili namna bora ya kutatua changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambapo wamesema bado jamii haina uelewa wa kutosha hivyo wameshauri elimu iendelee kutolewa.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Joseph Paul ameelekeza vyombo husika kuzichukua changamoto hizo na kwenda kuzifanyia kazi ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto huku akisisitiza ushirikiano.
“Michango hii mliyoitoa itasaidia sana kuboresha hizi kazi zetu za kutokomeza ukatili wa kijinsia na mambo haya tunayoyazungumza tunatakiwa tukayafanye kwa vitendo jamii yetu kwa kweli bado inahitaji msaada wa elimu juu ya haki zao kwahiyo tuendelee kushirikiana naamini kabisa kila mtu hapa ametoka na kitu kipya ambacho kwa nafasi yake ataenda kukifanyia kazi ambacho kwa ujumla vyote hivi zitaenda kusaidia katika mapambano ya kutokomea unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto”.
Kikao hicho kimefanyka Januari 26, 2022 ambacho kiliandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania ‘WFT’ ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto..