WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama amewataka Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma kufanya maandalizi na kusimamia utekelezaji wa mfumo mpya wa upimaji utendaji kazi kwa watumishi wa umma na taasisi zake (Opras).
Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara hizo zilizopo Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu mwelekeo wa mifumo ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.
Waziri Mhagama amesema kuwa Wizara yake imefanyia kazi agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa kwao wakati wa kikao chake na Mawaziri na Manaibu Waziri ambapo alieleza bayana kutoridhishwa na namna ambavyo mfumo huo wa ‘OPRAS’ unavyofanya kazi.
Katika kikao hicho na Mawaziri na Manaibu Waziri, Rais Samia alisema kuwa upimaji utendaji kazi kupitia OPRAS hauakisi hali halisi ya utendaji kazi kwa watumishi hali inayoleta hisia za kupendeleana au kuoneana. Pia matokeo ya upimaji utendaji kazi hayatumiki ipasavyo katika kufanya maamuzi ya kiutumishi.
Waziri Mhagama amesema katika kuendelea kutumia mfumo huo wa OPRAS uzoefu inaonesha kuwa mfumo huo ulioanzishwa mwaka 2004 una mapungufu hivyo kuamua kuchukua hatua za haraka za kuwaelekeza wataalamu wake kumaliza changamoto hiyo kwa kuja na mfumo mpya ambao utaanza kufanya kazi Julai 1, 2022.
” Katika kutekeleza agizo la Rais Samia tayari Ofisi yangu imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuja na mfumo wa Kielektroniki ambao utakua na manufaa Kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia uandaaji wa mikataba ya kazi kwa kuwa na malengo na shabaha za kila mtumishi zitawekwa katika mfumo Rafiki na kupunguza matumizi ya karatasi.
Mfumo huu unategemewa kuanza kutumika Julai 1, 2022, hivyo niwatake Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma kufanya maandalizi na kusimamia utekelezaji wa mfumo huu kikamilifu Kwa kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na Katibu Mkuu (Utumishi), Pia wahakikishe wanatenga bajeti kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa mfumo huu kwenye taasisi zao,” Amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa mfumo mwingine ni mfumo wa uwazi wa kupima utendaji kazi wa taasisi ambapo unajulikana kama mfumo wa mikataba ya utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi na ulianza rasmi mwaka 2018.
Amesema mfumo huu pia umefanyiwa kazi ili uwe wa Kielektroniki ni wa makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi za Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika inatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja.