Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akikagua maboresho yaliyofanyika katika madhari ya jengo la Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), wakati alipotembelea ofisi hizo jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akifafanua jambo kwa Uongozi wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), alipotembea kituo cha Huduma kwa wateja jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Paskas Samweli akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete kuhusu utoaji wa huduma katika kituo hicho wakati Naibu Waziri huyo, alipotembelea Ofisi za Kampuni, jijini Dar es Salaam. Wa tatu kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Albinus Manumbu.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Josephat Kagirwa alipomweleza kuhusu mipango mbalimbali ya Taasisi, wakati alipotembelea ofisi hizo jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akifafanua jambo kwa Menejimenti ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), alipotembea ofisi za Kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
…………………………………………………………………
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete ameitaka idara ya Masoko ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kufanya tafiti na kuja na mpango madhubuti wa bei za tiketi ili kuruhusu abiria wengi zaidi kutumia usafiri huo.
Akizungumza na Menejimenti ya ATCL Naibu Waziri Mwakibete amesema Serikali imewekeza fedha nyingi na inategemea shirika hilo kupata faida hivyo uwepo wa nauli zinazohimilika kutaongeza idadi ya abiria, pato na hatimaye shirika kuendelea kukua.
“Shirika hili limewekezwa fedha na idara kuu ambayo inaweza kufanya shirika hili kuendelea kibiashara ni idara ya masoko hivyo,mjipange vizuri ili kulifanya shirika kupata faida na kuweza kujiendesha’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amesema ni wakati sasa wa ATCL kuboresha kitengo cha huduma kwa wateja kwa kuhakikisha kama kuna taarifa za kuahirishwa kwa ndege abiria wanapewa taarifa mapema na kwa utaratibu unaoeleweka.
“Mara kwa mara kumekuwa na malalamiko ya wateja kupiga simu kuwa ndege zinaahirishwa na taarifa huzikuta pale pale Kiwanjani, hii haikubaliki, hili mlipe uzito na lisiendelee kutokea kwa mashali mapana na shirika” amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Albinu Manumbu amesema yako maboresho yanayoendelea kufanyika katika shirika hilo ikiwemo kuongeza idadi ya Watumishi katika kada mbalimbali ili kulifanya shirika kuwa na tija.
Manumbu ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuliamini Shirika na kuendelea kuwekeza kwani uwekezaji huo utalifanya shirika kuendelea kukuwa na kufanya biashara na hatimaye kupata mapato zaidi.
Naibu Waziri Atupele yuko mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kutembelea, kufahamiana na kuzungumza na viongozi na watumishi waliopo katika taasisi za Sekta ya Uchukuzi na pamoja na kukagua miradi ya kisekta.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)