……………………………………………………….
Kwa Ufupi: Benki ya NMB yaendelea kuwa benki kinara wa ufanisi nchini Tanzania
- Faida kabla ya kodi: TZS bilioni 420 – ongezeko la asilimia 41 kwa mwaka
- Faida baada ya kodi: TZS bilioni 289 – ongezeko la asilimia 39 kwa mwaka
- Mapato ya jumla yaongezeka kwa asilimia 18
- Uwiano wa gharama na mapato (CIR): 47%
- Thamani ya mali zote TZS 8.7 trilioni yapanda kwa asilimia 23
Ubora wa mpango mkakati, ongezeko la miamala ya wateja, morali ya hali ya juu wa wafanyakazi na uongozi thabiti, vyasaidia kuifanya NMB kuendelea kuwa benki kinara wa faida nchini.
Dar es Salaam. Januari 27, 2022. Benki ya NMB jana imetangaza matokeo ya uendeshaji wake ya mwaka 2021 ambapo imeweka rekodi nyingine ya utendaji kwa kupata faida kabla ya kodi ya TZS bilioni 420 (2020: TZS bilioni 301), kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 41.
Muundo wake wa biashara, na utekelezaji wa mipango kimkakati wake kwa nidhamu kubwa kumeendelea kuipa mafanikio ya umiliki wa soko, na hivyo kuimarisha nafasi yake ya uongozi wa kisekta nchini.
Faida ya TZS bilioni 289 baada ya kodi iliyopatikana mwaka kwa 2021 ni ongezeko la asilimia 39, kiasi ambacho ni zaidi ya faida yote ya mwaka 2020 (TZS 210) iliyovunja rekodi ya faida kuwahi kutengenezwa na benki yoyote nchini.
Ukuaji mkubwa wa faida ulitokana na ukuaji thabiti wa mapato kwa asilimia 18. Ukuaji huu ulitokana hasa na kukua kwa mapato yatokanayo na riba kwa asilimia 19, pamoja na ongezeko la mapato yasiyo ya riba kwa asilimia 15. Ongezeko hili la mapato ni kiashiria cha ukuaji thabiti wa mizania ya benki, mikopo kwa wateja, pamoja na ongezeko kubwa la miamala ya wateja wetu, kutokana na ubora na upatikanaji rahisi wa huduma zetu za kibenki.
Benki ya NMB pia imeendelea kuonyesha ufanisi mkubwa wa utendaji ambao uliboresha uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato hadi asilimia 47 kutoka asilimia 51 mwaka 2020, kiwango ambacho kipo ndani ya ukomo uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, wa asilimia 55.
Usimamizi makini wa mikopo na uhusiano mzuri na wateja uliimarisha ubora wa mali za benki na kuufanya uwiano wa mikopo chechefu kupungua hadi asilimia 3.2 mwezi Disemba mwaka 2021, kiwango ambacho ni kidogo kulinganisha na takwa la kikanuni la asilimia 5.
Benki imeendelea kuwa na mizania mathubuti ambayo ukuaji wake endelevu ni kielelezo cha uhusiano ulioimarika wa wateja katika maeneo ya kipaumbele ya biashara. Jumla ya mikopo iliongezeka kwa asilimia 13 mpaka TZS trilioni 4.6 baada ya ukopeshaji kukua katika sehemu kuu za soko hususani kwenye kilimo, biashara ndogo na za kati ikiwemo mikopo binafsi.
Kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba 2021, amana za wateja zilikua kwa asilimia 25 mpaka TZS trilioni 6.4 kulinganisha na TZS trilioni 5.3 Disemba 2020. Thamani ya mali zote mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa TZS trilioni 8.7 ikiwa ni ongezeko la asilimia 23 kutoka TZS trilioni 7 mwaka uliotangulia.
Akizungumzia matokeo hayo ya mwaka mzima, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema: “Ninajivunia sana na nimefurahishwa na matokeo tuliyoyapata kama timu, huku nikiwa na imani kuwa utekelezaji wa mikakati yetu kwa nidhamu, ukuaji endelevu wa biashara za wateja wetu, morali kubwa ya wafanyakazi ndani ya benki na uongozi imara, vitaendelea kuwa chachu ya kasi ya ukuaji wetu.”
Bi Zaipuna aliongeza kuwa, “ukuaji mkubwa wa biashara na utendaji wa kifedha wa benki yetu ni muhimu katika kuthibitisha dhamira yetu ya kuwa chombo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania:
- Kilimo tulikipa kipaumbele na mchango wetu katika sekta hii uliendelea mwaka jana, ambapo tulikuwa benki ya kwanza kuanzisha mfuko maalum wa kilimo kwa ajili ya kukopesha kilimo na mnyororo wake wa thamani kwa riba isiyozidi asilimia kumi.
- Pia tuliendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika programu mbalimbali za kijamii sambasamba na sera yetu ya masuala ya uwajibikaji kwa jamii. Kila mwaka benki ya NMB hutenga asilimia moja ya faida iliyopatikana baada ya kodi kwa ajili ya uwekezaji katika masuala ya kijamii, ambapo mwaka 2021, tukichangia zaidi ya TZS bilioni mbili kwenye masuala ya elimu, afya, elimu ya fedha na mazingira.
- Kulingana na ukuaji wetu endelevu, malipo yetu ya kodi kwa serikali yamekua mwaka hadi mwaka. Mwaka 2021, NMB ilitambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama mlipa kodi namba moja katika taasisi za fedha na mlipa kodi mkubwa wa tatu kwa makampuni yote makubwa nchini.
- Benki inaendelea kutoa huduma jumuishi za kifedha kwa mamilioni ya watanzania. Mwaka 2021 tulizindua suluhisho kadha kama Ushirika Afya, Spend2Save, Go Na NMB, Bima ya Mkono wa Pole (Mazishi) na Bima ya Jahazi ambazo zilirahisisha upatikanaji wa huduma na kuchangia ongezeko la wateja wa benki kufikia zaidi ya milioni nne.
Mafanikio ya ukuaji wa NMB na mchango wake mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania umeendelea kuifanya kinara wa ubora nchini kupitia tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Mwaka 2021, Benki ya NMB ilitunukiwa tuzo saba za kimataifa huku ikitangazwa kuwa Benki Bora na Salama Zaidi nchini Tanzania na Majarida ya Kimataifa.
“Tunawashukuru sana wateja wetu ambao thamani yao ni kubwa kwetu, tunawashukuru wanahisa, wadau wote na wafanyakazi wetu kwa kuendelea kutuunga mkono. Tunaendelea kushukuru Benki Kuu ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa sekta ya kibenki nchini. Tukiangalia siku za usoni, tuna matumaini makubwa ya safari iliyo mbele yetu. Tutatumia uwezo na misingi imara ya benki yetu kujenga zaidi thamani yake na kuleta ustawi wa pamoja kwa wadau wetu,” Bi Zaipuna aliitimisha.
#MWISHO