Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne A. Sagini akiwa katika nyumba iliyopoteza familia ya watu watano katika tukio la mauaji yaliyotokea Kijiji cha Zanka, wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na familia waliopoteza watu watano katika tukio la mauaji yaliyotokea Kijiji cha Zanka, wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Awahakikishia kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaendela kufanya uchunguzi wa tukio hilo na hatua za kisheria zitachukuliwa uchunguzi
ukikamilika.
Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ameitembelea familia iliyopoteza watu watano katika tukio la mauaji lililotokea tarehe 22 Januari 2022 na kuwapa pole na kuwahakikishia kuwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo na hatua za kisheria zitachukuliwa uchunguzi ukikamilika.
Akioneshwa kusikitishwa na kitendo cha mauaji ya wanafamilia hao, Naibu Waziri Sagini, amewahakikishia kuwa Jeshi la Polisi linaendela kutekeleza wajibu wao na kwamba uchunguzi unaendelea. Amesema kuwa mara uchunguzi utakapokamilika basi hatua za kisheria zitachukuliwa.
“Mhe, Makamu wa Rais ametoa maelekezo na Jeshi la Polisi linatekeleza wajibu wake wa kufanya uchunguzi, Sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunaungana na Watanzania wote kuwapa pole na Wizara itafanya wajibu wake wa kuwafikisha wahalifu mahakamani”
Naibu Waziri Sagini alisema hayo leo alipoitembelea familia hiyo katika Kijiji cha Zanka, Wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma.
Aidha amewasihi Watanzania kuwa na ushirikiano na wanafamilia wenzao kwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kusuluhisha migogoro yao na kuhakikisha wanatafutana iwapo wenzao hawaonekani ndani ya siku tatu ili kuhakikisha usalama na amani ya familia hata na jirani zao.
“Familia ziweke utaratibu wa kushirikiana utakaosaidia kuhakikisha kuwa kuna ulinzi na usalama wa kwenu ninyi na majirani. Haiwezekani mtu akapotea siku tatu bila ya familia kushtuka na kumuulizia”