Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS kwa mara ya kwanza leo umefanya mnada wa miti ya misaji (teak)kwa njia ya kielektroniki na kufanikiwa kuuza ploti zote kumi ilizotangaza kuziuza katika shamba la Longuza mkoani Tanga na Mtibwa, Morogoro kwa zaidi ya Sh1.3 bilioni.
Mfumo huu unapatikana katika njia ya tovuti (web) na MobileApp anasema Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Kitengo cha TEHAMA – TFS, Harold Chinpanha ambapo unawawezesha wateja kushiriki mnada pamoja na watumishi wa Wakala kufuatilia mchakato mzima.
“Hii ni mara ya kwanza kwa Wakala wa huduma za misitu kuendesha mnada kwa njia ya kielectroniki kwa kutumia mfumo uliobuniwa na kutengenezwa na wataalam wa ndani wa TEHAMA wa Wakala, na kufanikiwa kuuza kwa asilimia 100 miti yote iliyopimwa katika mashamba ya Mtibwa na Longuza,”
“Awali tulitarajia kukusanya jumla ya TShs.1,041,827,580.00 kwa bei ya kuanzia na baada ya kuuza tunatarajia kukusanya maduhuli ya Serikali zaidi ya TShs.1.3 bilioni ambapo Tsh 575,636,252.00 milioni tumeuza katika Shamba la Miti Mtibwa huku Longuza tukiingiza Tsh 748,982,951.50 milioni sawa na asilimia 127,” anasema Kamishina Msaidizi Mwandamizi Chinpanha.
Anaongeza kuwa kiasi hicho kimepatikana baada ya kuuza meta 1,963,331m za ujazo za miti hiyo. Mita 1,144.038 ziliuzwa Mtibwa na 819.293 shamba la Longuza.
Aidha, Chipanha anasema TFS inatambua TEHAMA ndio dunia ilipo na inakoelekea hivyo kuanzishwa kwa mauzo ya mnada wa Misaji kwa njia ya Kielektroniki kunalaenga kuachana na utaratibu wa kuuza missaji katika ofisi za mashamba husika ili kuongeza uwazi na ushindani.
Kampuni zote zilizoshinda zabuni hiyo, Mhifadhi Mwandamizi (SCO) Daniel Silima (Kaimu Meneja wa Leseni na Matumizi ya Rasilimali)i anasema zinatakiwa kulipa asilimia 25 ya thamani yote ndani ya siku tatu za kazi kuanzia siku ya mnada. Fedha hizo hazitarudishwa endapo mshindi atashindwa kulipia ujazo aliouziwa.
“Licha ya mnada huu kuwa wa kielectroniki kanuni za mnada zinabaki kama zilivyo, tayari tumeshawapa hati ya madai (bill) ya Mfumo wa Kielektroniki wa Makusanyo ya Serikali (GePG) wanunuzi wote. Asilimia 75 iliyobaki watalipa ndani ya siku kumi 14 baada ya mnada,” amesema Salima.
Mwanasheria wa TFS, Salome Rwiza anasema mnunuzi aliyeshinda mnada, atatakiwa kuondoa mazao aliyonunua ndani ya miezi miwili baada ya kumaliza kulipa malipo yote yanayostahili.
Zaidi ya kampuni Sita zilijitokeza na kushiriki kikamilifu kwenye mnada huo.